Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

JANUARI 9, 2024 JUMANNE. JUMA LA 1 LA MWAKA

By

on

JANUARI 9, 2024 JUMANNE. JUMA LA 1 LA MWAKA

Kijani

Zaburi. Juma 1

Mtakatifu: Adreano, Abate wa Kanterberi

Utume :   Alipelekwa Kanterberi (Uingereza) mwaka 668. Baadae alitawazwa    kuwa Abati wa Monasteri ya Mt. Augustino. Alifundisha fadhila na maandiko matakatifu. Alifundisha kwa miaka 39.

Kufariki: Mwaka 710.

Masomo

Somo 1. 1 Sam 1:9-20

Walipokwisha kula na kunywa huko Shilo Hana akainuka. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la Bwana. Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana, akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, “Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyu mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe. Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za Bwana, Eli akamwangalia kinywa chake. Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa. Ndipo Eli akamwambia, “Je! Utakuwa mlevi hata lini? Achilia mbali divai yako.” Hana akajibu, akasema, “Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni; mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za Bwana. Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa.” Ndipo Eli akajibu, akasema, “Enenda kwa amani na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba.” Naye akasema, “Mjakazi wako na aone kibali machoni pako.” Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakasali mbele za Bwana, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye Bwana akamkumbuka. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, “Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana.”

Wimbo wa Katikati

1 Sam 2:1, 4-5, 6-7, 8

  1. Moyo wangu wamshangilia Bwana, Pembe yangu imetukuka katika Bwana,
    Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu, Kwa kuwa naufurahia wokovu wako. (K)

K: Moyo wangu wamshangilia Bwana.

  • Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu.
    Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula, Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha.
    Naam, huyo aliyekuwa tasa amezaa watoto saba, Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika. (K)
  • Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu tena huleta juu.
    Bwana hufukarisha mtu naye hutajirisha; Hushusha chini tena huinua juu. (K)
  • Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani,
    Ili awaketishe pamoja na wakuu  Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu,
    Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana. (K)

Injili. Mk 1:21-28

Yesu na wanafunzi wake walishika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake, kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi.  Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu.” Yesu akamkemea, akisema, “Fumba kinywa, umtoke.” Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, “Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii!” Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya.

Tafakari

UWEZA WA MUNGU HUTUPONYA: Hana mjakazi wa Bwana amekuwa mtu wa sala. Ameweka nadhiri yake mbele ya Bwana ya kwamba akipata mtoto mwanamume atamtolea kwa Bwana. Hana hakati tamaa kwa maneno ya Eli alivyoambiwa mlevi wa divai, bali anadumu katika sala na katika hekima mbele ya Bwana. Bwana anasikia kilio chake na anampa mtoto Samweli. Mafundisho ya Yesu yaliwastaajabisha wanafunzi wake. Hii ni kwa sababu ya hekima yake iliyomfanya afundishe kwa amri. Hekima hii ni hekima ya kimungu. Pia kutokana na uweza wake wa kimungu, anawaamuru pepo wachafu na wanamtii. Wapendwa, ni kwa uweza wa Mungu Hana amepata mtoto, ni kwa uweza wa Mungu pepo wanaamriwa na wanatii. Hana amedumu katika sala, ametambua uweza wa Mungu na ndio maana harudi nyuma anavyoambiwa amelewa divai. Katika maisha yetu tukumbuke kuwa mfumbuzi wa changamoto zetu ni Mungu. Tunapokutana na vikwazo vya maisha tumkimbilie Yeye. Pia katika maisha, maneno yenye hekima ni tiba na yanadhihirisha uweza wa Mungu ndani yetu.

SALA: Ee Mungu, utujalie tudumu katika kukutumainia Wewe. Amina.

The post JANUARI 9, 2024 JUMANNE. JUMA LA 1 LA MWAKA appeared first on Claretian Publications.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2023, 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you