Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

DESEMBA 31, 2023; JUMAPILI: FAMILIA TAKATIFU

By

on

Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: YbS. 3:2-6, 12-14
Bwana amempa baba utukufu mintarafu wana, na kuithibitisha haki ya mama mintarafu watoto. Anayemheshimu baba yake atafanya malipizi ya dhambi, naye anayemtukuza mama yake huweka akiba iliyo azizi. Anayemheshimu babaye atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa. Anayemtukuza baba yake ataongezewa siku zake; akimsikiliza Bwana, atamstarehesha mamaye. Mwanangu, umsaidie baba yako katika uzee wake; wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake. Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana; kwa maana sadaka apewayo baba haitasahauliwa, na badala ya dhambi itahesabiwa kwa kukudhibitisha.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 128:1-5

  1. Heri kila mtu amchaye Bwana,
    Aendaye katika njia zake
    Taabu ya mikono yako hakika utaila;
    Utakuwa heri, na kwako kwema.
    (K) Heri kila mtu amchaye Bwana,
    aendaye katika njia zake.
  2. Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
    Nyumbani mwa nyumba yako.
    Wanao kama miche ya mizeituni
    Wakiizunguka meza yako. (K)
  3. Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana,
    Bwana akakubariki toka Sayuni.
    Uone uheri wa Yerusalemu.
    Siku zote za maisha yako. (K)

SOMO 2: Kol. 3:12-21
Ndugu zangu, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani. Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye. Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao. Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana. Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

SHANGILIO: Kol. 3:15, 16
Aleluya, aleluya,
Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu;
Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu.
Aleluya.

INJILI: Lk. 2: 22-40
Zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa, walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristu wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mkononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, kwa amani, kama ulivyosema kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, uliouweka tayari machoni pa watu wote; nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka kwa wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajiia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya, mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

TAFAKARI:
HABARI NJEMA KUHUSU FAMILIA: Leo ni siku ya kusema ukweli kuzihusu familia. Magonjwa yamezififisha familia. Familia nyingi zimekuwa katika maisha ya taabu sana. Ziko familia ambazo hata sasa wanahofu ya kusherehekea pamoja, kwa sababu kufurahi pamoja ni jambo muhimu sana kwa maisha yetu na tamaduni zetu. Familia ziko katika matatizo makubwa zaidi. Inawezekana kabisa hali hii ikawa ni mbaya zaidi kwa familia zilizo duni. Kumbe basi, katika familia duni jambo la msingi zaidi ni kuwa pamoja.
Lakini kuna habari njema kuhusu familia siku hii ya leo. Sitaki kusema kuwa katika Familia Takatifu mambo yalikuwa mazuri. Bila shaka ilikuwa na changamoto zake. Hebu tuwaze pale mtoto anatafutwa ili auawe na Herode. Hii familia haikuwa na makazi ya kudumu. Baada tu ya kuzaliwa, wanalazimika kuhamia Misri. Tatu mtoto Yesu alikuwa akikuwa na kuongezeka katika hekima, na alipofikia umri wa miaka 12, alipotea hekaluni kwa muda, na baadaye wakamkuta kule alipopaswa kuwepo katika hekalu. Alikuwa na wazee wenye hekima wakimsikiliza. Siku hiyo alikuwa anapaswa kufanya kazi ya baba yake.
Familia Takatifu ambayo Kanisa linaizungumzia leo sio kwamba ilikuwa kamilifu kabisa, kwamba hawakuguswa na matatizo na changamoto za maisha. Lakini ni kwa sababu kama familia zingine za kawaida kabisa, walizikabili changamoto za maisha yao, na kutafuta majibu sahihi ya changamoto zao. Zaidi ya hayo, Familia Takatifu ilibaki imeshikamana katika shida na katika raha pia. Walirudi nyumbani pale walipoona maisha ya mpendwa wao yako salama. Yosefu alijipatia mahitaji yake ya maisha pamoja na kuwa alikuwa ameendelea katika umri mkubwa. Maria naye alitimiza wajibu wake kama mama pamoja na umri wake kuwa mdogo. Wote wawili walifanya kile ambacho Bwana aliwataka wafanye. Na walifanya hayo kwa ushujaa mkubwa. Leo ni mwaliko kwa familia zote ulimwenguni kuishi maisha ya kishujaa kama hayo. Hamuitwi kudekezana, lakini mnaitwa kuishi maisha ya pamoja ingawa mnayo matatizo na changamoto zenu. Mnaitwa kuishi pamoja ijapokuwa mnavyo vikwazo katika maisha ya familia. Mnaitwa kuishi kulingana na mpango wa Mungu. Kama familia, mnaitwa kuwa vile mnavyopaswa kuwa. Familia ninyi ni kanisa dogo, ninyi mnaibeba sura ya kanisa. Na kanisa maana yake ni katika kila kitu, furaha, huzuni, na hofu. Na mwisho wa yote, zawadi mtakayoipata sio ya ulimwengu huu. Mtaishi pamoja na Mungu katika ulimwengu ujao.

SALA: Ee Mungu, tunaomba familia za kikristo iwe ni sehemu ambapo tunu za Injili zinasitawi. Kila mmoja, wazazi na watoto watimize wajibu wao, licha ya changamoto wanazokutana nazo. Amina.

The post DESEMBA 31, 2023; JUMAPILI: FAMILIA TAKATIFU appeared first on Claretian Publications.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2023, 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you