Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Dominika ya 31

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 03/11/2024

2024 NOVEMBA 3: DOMINIK YA 31 YA MWAKA

Rangi: Kijani
Zaburi: Juma III

SOMO 2. Kum 6 : 2-6#

Musa aliwaambia makutano: Upate kumcha Bwana, Mungu wako, kushika amri zake zote, na sheria zake, ninazokuamuru, wewe na mwanao, na mwana wa mwanao, siku zote za maisha yako; tena siku zako ziongezwe. Sikiza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali. Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako. 

WIMBO WA KATIKATI. Zab 18: 2-4, 47, 51

1. Wewe Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;
Bwana ni jabali langu,
Na boma langu na mwokozi wangu,
Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia.
Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu,
Na ngome yangu.
Nitamwita Bwana anayestahili kusifiwa,
Hivyo nitaokoka na adui zangu.

(K) Wewe Bwana nguvu zangu nakupenda sana.

2. Bwana ndiye aliye hai,
Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu
ampa mfalme wake wokovu mkuu,
amfanyia fadhili masiha wake. (K)

SOMO 2. Ebr 7 : 23 – 28

Wale walifanywa makuhani wengi, kwa sababu wazuiliwa na watu wasikae; bali yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee. Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu ; ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi zao hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake. Maana torati yawaweka wanadamu walio na unyonge kuwa makuhani wakuu; bali hilo neno la kiapo kilichokuja baada ya torati limemweka Mwana, aliyekamilika hata milele. 

INJILI. Mk 12: 28-34

Mmoja wapo wa waandishi alifika, akawasikia wakisemezana naye, akatambua ya kuwa amewajibu vema, akamwuliza, katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza? Yesu akamjibu, ya kwanza ndio hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu   ni Bwana mmoja, nawe, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi. Yule mwandishi akamwambia. Hakika, mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye; na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhabihu zote pia. Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo.

TAFAKARI

IMANI BILA MATENDO IMEKUFA
Mmesikia ikinemwa kuwa “matendo hunena zaidi kuliko matendo”. Matendo huonesha umaana na ulazima wa maneno yaliyotamkwa. Mmoja anapotamka kuwa rushwa ni mbaya basi anapaswa aoneshe kweli anaichukia rushwa kwa mfano wa maisha yake. Katika malezi ya watoto ndani ya familia na katika jamii ya mwanadamu msisitizo huwa ni katika kuwa mfano mzuri kwa matendo yetu mbele ya watoto. Hivyo si ajabu kuona mtoto mwenye mzazi mwenye tabia ya kusali akitoka katika familia ya wazazi wanaosali pamoja. Mfano mzuri ni Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu na wazazi wake ambao nao wamekwisha kuwekwa katika orodha ya Watakatifu ndani ya Kanisa. Leo tunakumbushwa neno hili: Imani bila matendo, imekufa.
Somo la kwanza linaanza kwa kutuonesha umuhimu wa matendo mema katika kudhihirisha ukaribu na muunganiko wetu na Mungu. Ili kuupata upendo wa Mungu na kufika katika nchi ya ahadi waisraeli wanapewa njia ya kupitia. Wanawekewa mbele yao vitu vya kuepuka kusudi upendo huo usiwapitie kando. Njia hiyo inajumuishwa katika Amri kumi ambazo kama tukiisoma sehemu inayoangulia Somo la kwanza la Dominika hii tutaona jinsi Musa alivyowapatia wana wa Israeli Amri hizo. Amri hizo haziwekwi kwao kama mlolongo wa maneno mazuri, bali kama njia ya kufuata. “Sikiza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa…” Mambo muhimu yanayosisitizwa: Kwanza ni kusikiliza. Kuwa tayari kulisikia Neno la Mungu, yaani kuyaweka mawazo yako yote na kuyakubali maneno anayokuambia.
Pili inasisitizwa kutenda. Maagizo tunayopewa na Mungu yanapaswa kutuingiza katika utendaji. Ni dokezo juu ya imani inayozaa matunda. Imani si jambo linalosimama bali ni tunu inayotuletea mabadiliko na kuzaa matunda. Mtume Yakobo anatuambia kwamba “imani isipokuwa na matendo imekufa nafsini mwake” (Yak 2:17). Tunapaswa kutekeleza kile tunachoambiwa katika Amri na maagizo tunayopatiwa na Mungu. Utekelezaji huo hutupeleka katika kuzaa matunda: “upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali.” Maagizo ya Mungu yananuia kutufikisha katika kuuonja wema wake. Ni njia sahihi ya kuyafikia mema hayo.
Mara nyingi amri na maagizo ya Mungu huangaliwa kama makatazo na namna hasi ambazo hutuondolea uhuru wetu. Lakini tukizama ndani katika tafakari tunatambua kuwa kwetu ni nyenzo za kuwa huru kweli na kuimarika katika upendo wa Mungu. Uhuru bandia wa kibinadamu hutufikisha katika utumwa wa mambo ya kidunia yanayoiharibu haiba yetu na kuuondoa utu wetu. Amri za Mungu zinanuia kutuepusha na matamanio ya uhuru bandia. Zinatuingiza katika ukaribu na Mungu na hivyo kuwa na jicho linaloyatazama mambo yote katika ukweli na kutuelekeza kutenda katika ukweli, namna ambayo inatupatia uhuru wa kweli. Ulimwengu na vyote vilivyomo ndani yake ni mali ya Mungu. Uwepo wake ndani mwetu unatuunganisha naye yeye aliye chanzo na mwezeshaji wa yote na hivyo kutupitisha katika ukweli.
Kama kumpenda Mungu ni kuzisikiliza amri zake basi namna ya kuzishika amri hizo ni kuzimwilisha katika matendo yetu ya upendo kwa jirani zetu. Matunda ya upendo wetu kwa Mungu yanathibitishwa na ukarimu wetu kwa wenzetu. Tendo la kuamini na kuzishika amri za Mungu linauonesha upendo wetu kwa Mungu. Upendo huo unakamilika na kukua katika upendo wetu kwa jirani zetu. Injili Takatifu inaufafanua upendo huo ambao ni mithili ya sehemu mbili za sarafu. Kristo anaonesha kuwa kiini na msingi wa amri zote umejikita katika namna hiyo ya upendo: kwa Mungu na kwa jirani, namna mbili za upendo ambazo haziwezi kutenganishwa. Ukaribu wetu na Mungu unatuunganisha na wenzetu.
Tendo la upendo kwa jirani zetu linaifunua haiba ya undugu wetu wa kikristo. Kwa kuzitii amri za Mungu mmoja anathibitisha kuungana naye na kukiri kuwa ni Baba yake. Hii ni namna ya kuikiri nafasi ya Mungu Baba kama chanzo na sababu ya uwepo wake. Imani hii inaiweka wazi hadhi yetu ya kuwa wana wa Mungu katika Mwana wake mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo. Haiba ya kuwa wana ndiyo inatuunganisha sisi kama ndugu na hivyo undugu wetu unapata msingi wake katika sifa hiyo ya kuwa wana katika Kristo. Hivyo paji la upendo wetu kwa Mungu ambalo linatuunganisha naye kama Baba yetu linatuunganisha na ndugu zetu na kutusukuma kudhihirisha upendo wetu kwa Mungu kwa matendo mema kwa ndugu zetu. Hiyo ndiyo namna ya kuzaa matunda na kuzitimiza amri za Mungu.
Kuhani wetu mkuu Kristo, tofauti na makuhani wa Agano la kale anatuonesha kwa vitendo namna muunganiko na Mungu unavyojidhihirisha katika muunganiko wetu na wenzetu. Namna yake hii inapata tija kwa sababu ya udumifu wake “kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka”. Udumifu huu unafunua na kudhihirisha upendo wa Mungu kwetu, upendo unaodumu milele. “Kwa maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii, aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lolote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu.” Huyu ni yule ambaye ameunganika na Mungu na hivyo muunganiko huo ni chanzo cha matendo yote katika uhuru na ukweli.
Sisi nasi kwa kuungana na Kristo tunaelekezwa katika kuufunua na kuudhihirisha upendo huo udumuo milele. Sadaka ya Kristo inapata nguvu zaidi kwa namna ilivyotolewa. Anajitoa nafsi yake mwenyewe. Kitendo cha kujitoa nafsi yake kinamtukuza juu kuliko sadaka za zamani na kutufunulia jinsi alivyokuwa tayari kujisadaka bila kujibakisha kwa ajili ya wenzake. Hicho ndicho kielelezo chetu cha upendo wa kikristo, yaani upendo ambao si wa kujitafuta ndani ya nafsi yako bali kujitoa nafsi yako na kujitafuta katika wengine walio pembeni yangu hasa wale ambao wana kiu ya upendo na faraja ya Mungu. Upendo wangu kwa Mungu unaotokana na muunganiko wangu na yeye unabubujika katika matendo yangu ya kindugu kwa wenzangu.
Kwa kujitoa kwake mara moja Kuhani wetu Mkuu ametupatia tumaini la milele katika sadaka yake moja na ya pekee kwa ajili ya uzima wa binadamu wote. Hivyo ni wajibu wetu kuipokea na kujimithilisha na sadaka hii inayokuwa mbele yetu kila siku kwa namna ya kipekee katika Ekaristi Takatifu sana. Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya upendo inatuunganisha na upendo wa Kristo na kutufanya kumithilika naye na hivyo kuwa nguvu kwetu ya matendo mema ya kikristo. Inakuwa kwetu nguvu ya kulisikiliza Neno la Mungu na kwenda kulitekeleza katika maisha yetu ya kila siku. Kusudi la Mwana wa Mungu, aliyekufa msalabani na kufufuka lilikuwa ni kuwapatia uzima watu wote. Ni wajibu wetu kujishikamanisha na sadaka hiyo ili kupata nguvu na ujasiri wa kuufunua upendo wa Mungu kwetu kwa matendo yetu.

SALA: Ee Mungu ufanye imani yetu idhihirike katika matendo yetu.

The post Masomo ya Misa Dominika ya 31 appeared first on CLARETIAN PUBLICATIONS-EAST AFRICA.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2023, 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you