Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Septemba 6

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 06/09/2024

2024 SEPTEMBA 6: IJUMAA-JUMA LA 22 LA MWAKA

Mt. Magnus
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 2

Somo 1. 1 Kor 4:1-5

Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu. Lakini, kwangu mimi, si kitu kabisa nihukumiwe na ninyi, wala kwa hukumu ya kibinadamu, wala sijihukumu hata nafsi yangu. Maana sijui sababu ya kujishitaki nafsi yangu, lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo; ila anihukumuye mimi ni Bwana. Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu.

Wimbo wa Katikati. Zab 37:3-6, 27, 28, 39-40

1. Umkabidhi Bwana njia yako.
Pia umtumaini, naye atafanya.
Ataitokeza haki yako kama nuru,
Na hukumu yako kama adhuhuri.

(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.

2. Umtumaini Bwana ukatende mema,
Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
Naye atakupa haja za moyo wako. (K)

3. Jiepue na uovu, utende mema,
Na kukaa hata milele.
Kwa kuwa Bwana hupenda haki,
Wala hawaachi watauwa wake. (K)

4. Na wokovu wa wenye haki una Bwana;
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa;
Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa;
Kwa kuwa wamemtumaini Yeye. (K)

Injili. Lk 5:33-39

Mafarisayo na waandishi walimwambia Yesu, “Wanafunzi wa Yohane hufunga mara nyingi, na kuomba dua; na kadhalika wanafunzi wa Mafarisayo; lakini wanafunzi wako hula na kunywa!” Lakini Yesu akawaambia, “Je! Mwaweza kuwafanya wafunge walioalikwa arusini, akiwapo bwana arusi pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi, ndipo watakapofunga siku zile. Akawaambia na mithali, “Hakuna akataye kiraka cha vazi jipya na kukitia katika vazi kuukuu; na kama akitia, amelikata lile jipya, na kile kiraka cha vazi jipya hakilingani na lile vazi kuu kuu. Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama akitia, ile divai mpya itavipasua vile viriba, divai yenyewe itamwagika, na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya sharti kutiwa katika viriba vipya. Wala hakuna anywaye divai ya kale akatamani divai mpya; kwa kuwa asema, ‘Ile ya kale ndiyo iliyo njema.’”

TAFAKARI

MAANA HALISI YA KUFUNGA: Yesu aliulizwa aeleze ni kwa sababu gani wanafunzi wake hawafungi na kusali kama wanafunzi wa Yohane na wale wa mafarisayo? Naye aliwajibu ya kwamba watu walio katika sherehe ya bwana harusi hawawezi kuzuiliwa kula chakula. Wanayo furaha nyingi ya kusherekea pamoja na bwana na bibi harusi. Hivyo wale waliokuwa wanafunga walifanya hivyo kama sehemu ya kujinyima ili kumtafuta Mungu kulingana na sheria yao. Ila wanafunzi wa Yesu hawakuhitaji kufunga kwa sababu walikuwa na Bwana arusi. Kwa kweli anawaelezea ya kwamba kuna wakati atakapoondolewa miongoni mwao kwa sababu yoyote ile, ndivyo hata wao watahitaji kufunga, kuomba na kumtafuta Mungu. Katika nafasi hiyo, Yesu anatutaka sisi kupenda au kufuata mafundisho ya Agano Jipya. Watu waliompokea Kristo katika kanisa lake wamekuwa wapya na iliwabidi washikilie mafundisho mapya na kumvaa Kristo ambaye ndiye divai mpya. 

SALA: Ee Bwana utujalie neema ya kuishi maisha mapya yaliyosimikwa juu ya Agano Jipya.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2023, 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you