Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Septemba 5

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 05/09/2024

2024 SEPTEMBA 5: ALHAMISI-JUMA LA 22 LA MWAKA

Mt. Teresa wa Kalkuta
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Juma 2

Somo 1. 1 Kor 3:18-23

Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima. Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao. Na tena, Bwana anayafahamu mawazo ya wenye hekima ya kwamba ni ya ubatili. Basi, mtu ye yote na asijisifie wanadamu. Kwa maana vyote ni vyenu; kwamba ni Paulo, au Apolo, au Kefa; au dunia, au uzima, au mauti; au vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu; nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.

Wimbo wa Katikati. Zab 24:1-6

1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.

(K) Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana.

2. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili,
Wala hakuapa kwa hila. (K)

3. Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)  

Injili. Lk 5:1-11

Makutano walipomsonga Yesu wakilisikiliza neno la Mungu, Yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti, akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao. Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni. Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, “Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.”  Simoni akajibu akamwambia, “Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.” Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, “Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana.” Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata; na kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.” Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata.  

TAFAKARI

TUMSIKILIZE KRISTO ANAYETUFUNDISHA NA KUTUELEKEZA: Petro alikuwa mvuvi mzoefu kama hakupata samaki asingalikuwa na njia ya kuishi. Katika ziwa la Genesareti walivua samaki nyakati za usiku, wakati huu wamejitahidi kuvua usiku kucha bila kupata chochote. Asubuhi wanakutana na Kristo, anaingia katika chombo chao na kuwafundisha watu. Kisha anawaambia; “Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.”  Simoni akajibu akamwambia, “Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.” Kama umefanya kazi usiku kucha na hujafanikiwa kwa kweli hutajisikia vizuri asubuhi. Petro alikuwa amechoka na anasafisha nyavu zake baada ya kutafuta Samaki usiku kucha bila kupata. Je! aliamini kuwa angalipata samaki?
Petro na wenzake walitii walivyoagizwa na Kristo. Basi hata sisi katika shughuli zetu za kila siku tujitahidi kuisikiliza sauti ya Kristo inayotualika kutenda jambo fulani bila kusahau kila siku kwamba tunalikwa kumwongokea Mungu. 

SALA: Ee Bwana Yesu utuwezeshe kuendelea kuisikiliza sauti yako na kuitii.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2023, 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you