Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Mei 1

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 01/05/2024

2024 MEI 1 : JUMATANO-JUMA LA TANO LA PASAKA

MT. YOSEFU MFANYAKAZI
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 1

Somo 1. Mdo 15:1-6

Siku zile, walishuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka. Basi baada ya Paulo na Barnaba kushindana na watu hawa na kuhojiana nao sana, ndugu wakaamuru kwamba Paulo na Barnaba na wengine miongoni mwao wapande kwenda Yerusalemu kwa mitume na wazee kwa habari ya swali hilo. Basi, wakisafirishwa na kanisa, wakapita kati ya nchi ya Foinike na Samaria, wakitangaza habari za kuongoka kwao mataifa; wakawafurahisha ndugu sana. Walipofika Yerusalemu wakakaribishwa na kanisa na mitume na wazee, nao wakawaeleza mambo yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao. Lakini baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walioamini wakasimama wakisema, Ni lazima kuwatahiri na kuwaagiza kuishika torati ya Musa. Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno hilo.

Wimbo wa Katikati. Zab 122:1-5

“1. Nalifurahi waliponiambia
Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama
Ndani ya malango yako, ee Yerusalemu. (K)

2. Ee Yerusalemu uliyejengwa
Kama mji ule ulioshikamana,
Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana. (K)

3. Ushuhuda kwa Israeli,
Walishukuru jina la Bwana.
Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
Viti vya enzi vya mbari ya Daudi. (K) “

(k) Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana.

Injili. Yn 15:1-8

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.

TAFAKARI

KAZI HUMHESHIMISHA MWANADAMU: Kanisa linaungana leo na watu wengine kusherehekea siku ya wafanyakazi ulimwenguni. Aidha Kanisa linakumbuka mchango wa Papa Pius XII aliyetambua mchango wa wafanyakazi na vyama vyao. Kwa namna ya pekee alivisifu vyama vya wafanyakazi vya kikristo kwa kueneza na kuulinda mwenendo wa kikristo kati ya wanachama na kuuneza ufalme wa Mungu. Papa Pius XII aliiweka sikukuu ya Mt. Yosefu mfanyakazi ili awe mfano wao. Lengo likiwa kwamba wafanyakazi na vyama vyao viwe vyanzo vya kueneza amani na mapatano ya haki na upendo badala ya kuwa vichocheo vya visa vya uovu na chuki. Hivyo basi sikukuu ya Mt. Yosefu Mfanyakazi ilete maana ya kiroho ya kazi zetu. Hii ni kwa sababu msingi wa kazi ni Mungu mwenyewe ambaye alifanya kazi ya uumbaji kwa siku sita. Nasi tufanyapo kazi tunashiriki katika kazi ya uumbaji na kuifanya dunia mahali pazuri pa kuishi. Tuchukue nafasi hii kuwaombea wafanyakazi wote ulimwenguni ili Mungu azibariki kazi zao na zizae matunda mema kwa ajili ya kueneza ufalme wa Mungu.

SALA: Ee Mungu uzibariki kazi za mikono yetu.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2023, 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you