Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 21/02/2024
2024 FEBRUARI 21 JUMATANO: JUMA LA 1 LA KWARESIMA
Mt. Petro Damiano Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Urujuani
Zaburi: Juma 1
Somo 1. Yon 3: 1-10
Neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili, kusema, Ondoka uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukaihubiri habari nitakayokuamuru. Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu, Yona akaanza kuuingia mji kwa mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata yeye aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake, kusema. Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng’ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili tusiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.
Wimbo wa Katikati. Zab 51:3-4, 12-13, 18-19
1. Ee Mungu, unirehemu,
Sawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu. (K)
(K) Moyo uliovunjika na kupondeka,
Ee Mungu, hutaudharau.
2. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)
3. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika,
Moyo uliovunjika na kupondeka. (K)
Injili. Lk 11: 29-32
Makutano walipokuwa wakimkusanyikia, Yesu alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka nchi za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.
TAFAKARI
NI VIZURI KUMSIKILIZA KRISTO KULIKO KUNGOJEA ISHARA: Katika kipindi hiki cha Kwaresma, Mama Kanisa anaendelea kutusihi kufanya mabadiliko. Mama Kanisa anatupa mfano wa watu wa Ninawi ambao kutokana na mahubiri ya Yona wanayabadili maisha yao maovu na wanamgeukia Mungu. Mungu alivyoona matendo yao ya kuwa wamebadilika, alighairi neno lile ya kwamba atawatenda. Kuokoka kwa watu wa Ninawi kunatokana na kubadili mienendo yao. Katika Injili, tunakumbushwa na Yesu kwa mfano wa kizazi kinachotafuta ishara. Yesu anatoa mifano ya Yona aliyekuwa ishara kwa watu wa Ninawi na Malkia wa Kusini ambaye alikuja aisikie hekima ya Sulemani. Yesu anasema kuwa yeye ni mkubwa kuliko Yona na Sulemani. Yeye ndiye mwenye yote katika wote hivyo tumsikilize. Wapendwa Taifa la Mungu, katika ulimwengu tunaoishi tumepata fursa ya kulisikia Neno la Mungu, yatupasa baada ya kulisikiliza, tubadili mienendo yetu tusisubiri mpaka ujio wa pili wa Yesu, tusisubiri mpaka siku ya hukumu. Mabadiliko ni yaanze sasa.
SALA: Ee Bwana, tunakuomba utufanye daima tusiwe watu wa kutafuta ishara, tuwe tayari kubadili mienendo yetu ili tustahilishwe kufika kwako, amina.