Masomo ya misa

Masomo ya Misa: Dominika Kristu Mfalme

By

on

Rangi: Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1. Dan 7: 13-14

Niliona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie, mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa. 

WIMBO WA KATIKATI: Zab 93: 1-2, 5

“1. Bwana ametamalaki, amejivika adhama,
Bwana amejivika, na kujikaza nguvu.

(K) Bwana ni mfalme, amejivika taji.

  1. Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike;
    Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani.
    Wewe ndiwe uliye tangu milele. (K)
  2. Shuhuda zako ni amini sana;
    Utakatifu ndio uifaao nyumba yako.
    Ee Bwana, milele na milele. (K)”

SOMO 2. Ufu 1: 5-8

Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina. Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam, Amina. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.

INJILI. Yn 18: 33-37

Pilato aliingia ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia: Je! Wewe ni mfalme wa Wayahudi? Yesu akamjibu, wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu? Pilato akajibu, Ama! Ni Myahudi mimi! Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini? Yesu akajibu, ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa. Basi Pilato akamwambia, Wewe u mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu. 

TAFAKARI

“TAFAKARI: Leo tunaadhimisha Dominika ya 34 ya Mwaka wa Kanisa, ambapo Mama Kanisa anasherehekea Sherehe ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme. Ni sherehe ambayo ilianza rasmi mwaka 1925 wakati Papa Pius XI alipoona matumizi mabaya ya madaraka ya wafalme wa dunia hii. Wafalme wa dunia ambao walijaa unyanyasaji, dhuluma na ukatili. Wafalme wasiokuwa na upendo. Hivyo Papa Pius XI alianzisha Sherehe hii ili kutoa sura ya Kristo Mfalme ambaye ni Mfalme wa amani; Mfalme mwenye upendo; Mfalme mwenye huruma; Mfalme mnyenyekevu. Mfalme asiyetumia mabavu kutawala, asiye na jeshi. Kristo, Mfalme asiye na taji wala vazi la dhahabu. Kristo, Mfalme aliyetoa uhai wake kwa ajili ya watu wake. Na huyu ni mfalme ambaye ufalme wake si wa dunia hii. Kristu ni Mfalme ambaye ufalme wake si wa dunia. Akimjibu Pilato alisema: “”Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa””(Yoh 18:37). Kristo ni Mfalme ambaye adui yake mkubwa si mwanadamu bali ni Ibilisi na nguvu zake zote. Lakini, Kristo Mfalme atakapokuja katika ufalme wake “”Atawaweka maadui wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti””(1Kor 15:25-26).
Kristu Mfalme wetu ni Mfalme wa amani na upendo. Anatualika sisi tuishi kwa amani na upendo, akisema “”Pendani; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi…Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu””(Yoh 13:34; 14:27). Tunaposherehekea Sherehe ya Kristo Mfalme, tunaalikwa tutambue kwamba Yeye ni Mfalme na mtawala wa maisha yetu. Yeye ni mchungaji wetu ambaye tukimfuata hatutapungukiwa na kitu. Tuungane na Kristo Mfalme wetu ili siku moja tuweze kutawala pamoja naye.”

SALA: Tumwombe Kristu atukumbuke na atukaribishe sisi pia katika ufalme wake wa mbinguni.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2025 2024 2023 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you