Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 01/09/2024
2024 SEPTEMBA 1: DOMINIKA YA 22 YA MWAKA
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 1
Somo 1. Kum 4 :1-2, 6-8
Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu, niwaamuruzo. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo. |
Wimbo wa Katikati. Zab 15: 2-5
1. Bwana, ni nani atakayefanya maskani yake (K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako? 2. Ni yeye ambaye hakumtenda mwenziwe mabaya, 3. Ni yeye ambaye hayabadili maneno yake, |
Somo 2. Yak 1: 17-18, 21-22, 27
Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka. Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake. Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu. Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii. Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa. |
Injili. Mk 7: 1-8, 14-15, 21-23
Mafarisayo, na baadhi wa waandishi waliotoka Yerusalemu, wakakusanyika mbele ya Yesu wakaona wengine katika wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa. Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao; tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yapo mambo mengine waliyopokea kuyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba. Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza, Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi? Akawaambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu. Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu. Akawaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivu, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi. |
TAFAKARI
SHERIA YA KRISTO INAJENGA UTU MPYA SALA: Ee Mungu utujalie tukuabudu kwa moyo na roho. |