Masomo ya misa

Masomo ya Misa Dominika ya 30

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 27/10/2024

2024 OKTOBA 27: DOMINIKA YA 30 YA MWAKA

Rangi: Kijani
Zaburi: Juma II

SOMO 1. Yer 31: 7-9

Bwana asema hivi, Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee Bwana, uwaokoe watu wako mabaki ya Israel. Tazama, nitawaleta toka nchi ya kaskazini, na kuwakusanya katika miisho ya dunia, na pamoja nao watakuja walio vipofu, na hao wachechemeao, mwanamke mwenye mimba, na yeye pia aliye na utungu wa kuzaa; watarudi huko, jeshi kubwa. Watakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyoka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 126

1. Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
Na ulimi wetu kelele za furaha.

(K) Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa tukifurahi.

2. Ndipo mataifa waliposema,
Bwana amewatendea mambo makuu,
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi. (K)

3. Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini.
Wapandao kwa machozi,
Watavuna kwa kelele za furaha. (K)
4. Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda.
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Aichukuapo miganda yake. (K)

SOMO 2. Ebr 5: 1-6

Ndugu, kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu, na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi. Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni. Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. Kama asemavyo mahali pengine, Ndiwe kuhani milele Kwa mfano wa Melkizedeki.

INJILI. Mk 10: 46-52

Yesu alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama akasema, mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita. Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.

TAFAKARI

KRISTO KUHANI MKUU: KWA NJIA YAKE TUMEUHISHWA UPYA
Mwanadamu katika hali ya mahangaiko na udhaifu hutafuta faraja. Hali hiyo inapopatikana, yaani kuwa na faraja au nafuu mwanzo mpya huonekana. Lakini tukijiuliza sababu za mahangaiko au udhaifu fulani tunaona haraka kuwa vyote husababishwa na upungufu fulani. Katika hali hiyo, na tukizingatia kuwa mwanadamu alipoumbwa aliumbwa katika hali ya ukamilifu, hali ya udhaifu au mahangaiko huashiria upungufu fulani katika ukamilifu wake. Mafundisho ya Kanisa yanatuonesha kuwa taabu hizi na masumbuko zilianza na na anguko la kwanza la mwanadamu. Anguko hilo limejumuishwa katika kitendo cha kumuasi mwenyezi Mungu. Hivyo tunaona kuwa taabu na mahangaiko yanamfika mwanadamu kwa sababu ya kuufukuza uwepo wa Mungu ndani yake na hivyo kuukosa msingi, chanzo na sababu ya uwepo wake na kazi yote ya uumbaji.
Historia nzima ya wokovu wa mwanadamu inajikita katika kuirekebisha hali hiyo. Somo la kwanza linaanza kwa kutuonesha jinsi Mungu anavyoanza kuwaunda upya watu wake. Hii ni baada ya uasi wao ambao uliwapeleka utumwani. Sehemu hii ya kitabu cha Nabii Yeremia huitwa «kitabu cha faraja». Nabii Yeremia aliishi wakati wa kipindi hiki kigumu ambapo alishuhudia kuharibiwa kwa mji wa Yerusalemu kulikotimizwa na jeshi la Babeli. Yerusalemu ilikuwa ni ishara ya uwepo wa Mungu kwa taifa la Israeli. Katika mji huu waliona ufahari wote wa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Uharibifu wa mji huu, muhimu kama ulivyokuwa, umewaachia uchungu mkubwa sana. Lakini ujumbe wa faraja wanaoupata ni sababu ya kupata tena nguvu. “Tazama, nitawaleta toka nchi ya kaskazini, na kuwakusanya katika miisho ya dunia”. Mwaliko wa Bwana Mungu kwao unawahakikishia wokovu na kuanza upya tena.
Bwana ananuia kuwakomboa hao wanaoitwa «mabaki ya Israeli». Pengine hali zao zinaweza kuonesha udhaifu, maana tunaambiwa “pamoja nao watakuja vipofu, na hao wachechemeao, mwanamke mwenye mimba, na yeye pia aliye na utungu wa kuzaa.” Lakini Mungu anaanzisha familia mpya kupitia watu hawa. Mwenyezi Mungu anawaahidia ulinzi na uongozi wake hadi kufikia ukamilifu. “Nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyooka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu.” Mungu anapojitambulisha katika sura ya baba anaifunua haiba yake kama chanzo na tegemeo la uumbaji wote. Haiba hii ni muhimu katika kukazia umuhimu wa uwepo na utegemezi wa mwanadamu kwa Mungu.
Somo la pili linatuonesha Kristo aliye Kuhani Mkuu na kwa njia yake tunahuishwa upya. Huu ni wito kwa wanadamu wote kuiona nafasi nyeti ya Kristo katika kuufanya hai uwepo wa Mungu na hivyo kumfanya Yeye, yaani Mungu, kuwa sehemu muhimu ya uwepo wa kazi yote ya uumbaji. Kristo kama kuhani wetu wa Agano jipya anatambulishwa katika Yeye “aliyetwaliwa katika wanadamu.” Hii inaturudisha Dominika iliyopita ambapo tulimwona Yeye aliye Kuhani wetu Mkuu akishiriki katika ubinadamu wote kwa hali zote. Yeye alizichukua taabu na mahangaiko yetu katika mwili wake. Katika ushiriki huo anajitoa nafsi yake kuwa sadaka ya upatanisho wetu na Mungu. Uwepo wake huu wa kikuhani unaoneshwa vizuri katika namna yake ya umungu na ubinadamu na hivyo kwa njia yake umungu na ubinadamu, uliotengana kwa sababu ya dhambi, unaunganishwa tena.
Ukuhani wa Kristo mfufuka unajionesha kama nyenzo ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika taabu na udhaifu wake. “Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake” (Ebr 2:17). Kwa kuyachukua madhaifu yetu katika mwili wake na kuyagongomelea katika mti wa msalaba anafufuka mzima, katika mwili wa utukufu, mwili unaooesha ushindi wa uhai dhidi ya kifo na mauti. Katika Yeye tunaupata upya wa ubinadamu wetu na hivyo tunaunganishwa tena na Mungu. Kristo Kuhani Mkuu anakuwa kwetu sababu ya kuunganika tena na Mungu na hivyo kupata hakika ya faraja aliyoiahidi katika somo la kwanza kwamba “nitawaongoza, nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyooka; katika njia hiyo hawatajikwaa.”
Uwepo wa Kristo unaonesha kwa vitendo uwepo wa wema wa Mungu unaorudisha matumaini na mwanzo mpya kwa mwanadamu. Nafasi hiyo ya Kristo inajionesha katika uponyaji anaomfanyia Bartimayo mwana wa Timayo. Kwa njia ya uponyaji huu wa kimwili kwa kipofu Bartimayo tunapaswa kuzama ndani na kuuona uponyaji wa kimasiha wa Kristo ambao ni kwa ajili ya wokovu wetu. “Enenda zako, imani yako imekuponya.” Dokezo hili la imani kutoka kwa Kristo linasakafia umuhimu wa paji la imani katika kuupokea uponyaji huo wa kimasiha ndani ya roho zetu. Imani hiyo huchagizwa na uelewa wetu wa ndani wa haiba ya Kristo na nafasi yake katika maisha yetu wanadamu. Hii inamaanisha kwamba, tusipomwelewa Kristo na haiba yake ya ukombozi inayodadavuliwa katika somo lake la pili ni aghalabu kuomba uponyaji wake. Baada ya uponyaji tunaambiwa: “akamfuata njiani.” Hapa tunaiona nafasi ya mmoja anayefunuliwa uelewa wake wa ndani, anamtambua Kristo na nafasi yake na hivyo anayatoa maisha yake ili kuambatana naye.
Mwanadamu anapoamua kuasi na kumwacha mwenyezi Mungu huangukia katika upofu na kushindwa kutembea barabara. Mara nyingine huwa anajitutumua kwa kujikinai kuyafanikisha yote kwa uwezo wake lakini katika uhalisia taraja yake humwingiza katika ama majibu ya kupita kwa kitambo kifupi tu au kutokupata kadiri ya matarajio yake. Namna hii humwingiza mwanadamu katika utumwa mbaya zaidi ya ule wa kisiasa walioupata wana wa Israeli. Zama za falsafa ya “uangaziwaji” au Illumination ilimkuza mwanadamu katika kiburi chake na kufikiri kuwa akili yake inayo uwezo wa kumfikisha katika elimu yote. Akiwa amejisahau katika ukomo wa asili yake mang’amuzi mengi ya binadamu ambayo yalimwondoa mwenyezi Mungu yamempeleka katika balaa. Matokeo yake ni vita na vurugu zisizokwisha, dhuluma ya utu wa mtu kati ya jamii moja moja na ulimwengu mzima n.k.
Leo Kristo anatuuliza kila mmoja kwa nafasi yake: “Wataka nikufanyie nini?” Ni vema jibu letu likawa kama la Bartimayo mwana wa Timayo: “Mwalimu wangu, nataka nipate kuona.” Jibu hili linafanana na ile hekima ya Solomoni pale alipopata nafasi ya kuomba chochote kwa Mungu na jibu lake nikawa: “nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?” (1Fal 3:9). Hekima hii inayoombwa na Solomoni hufanana na hamu ya Bartimayo ya kutaka kuona. Mwanadamu amejaliwa karama na vipaji mbalimbali. Mwenyezi Mungu amewekeza katika kila mmoja mmoja wetu kwa makusudi ya kuujenga vema ulimwengu huu. Tunapoitoa na kuidharau hekima ya Mungu mara nyingi tunajiingiza katika matumizi mabaya ya nafasi zetu na matokeo yake ni unangamizi kwa mtu binafsi na jamii nzima.

SALA: Ee Bwana Yesu utufanye tuweze kuona kiimani ili tuyatukuze matendo yako makuu.

The post Masomo ya Misa Dominika ya 30 appeared first on CLARETIAN PUBLICATIONS-EAST AFRICA.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2025 2024 2023 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you