Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 03/08/2024
2024 AGOSTI 5: JUMATATU-JUMA LA 18 LA MWAKA
KUNG’ARA B. W. YESU KRISTU
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 2
Somo 1. Dan 7:9-10, 13-14
Mimi nilitazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa. Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa. |
Wimbo wa KAtikati. Zab 97:1-2, 5-6, 9
1. Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie, (K) Bwana ametamalaki, juu sana kuliko nchi yote. 2. Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana 3. Maana wewe, Bwana, ndiwe uliye juu, |
Somo 2. 2 Pet 1:16-19
Hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, “Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu. Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing’aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu. |
Injili. Mk 9:2-10
Yesu aliwatwaa Petro, na Yakobo, na Yohane, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao; Mavazi yake yakimeta-meta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu. Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi ni vizuri sisi kuwapo hapa; Na tufanye vibanda vitatu, Kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Maana hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi. Kisha likatokea, wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye. Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu. Wakalishika neno lile, wakiulizana wao kwa wao, huko kufufuka katika wafu maana yake nini? |
TAFAKARI
TUSHIRIKI UTUKUFU WA YESU: Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya kung’ara Bwana wetu Yesu Kristo. Tukio hili la kung’ara kwa Bwana wetu Yesu Kristo linatufunulia sisi kujua thamani ya wito wetu wa Kikristo; kwamba tumeitwa ili kumwiga Kristo: kubadilika kutoka hali ya kale ya utu wetu na kuwa watu wapya, tunaong’ara si kwa sura za nje bali kwa sura za ndani, roho zetu. Tukio hili litupe hamu ya kubaki tumeungana na Yesu kama alivyotamani Petro kubaki pale mlimani. Tukio hili la litukumbushe kwamba kuna sauti moja tu ya kweli ya kuisikiliza na kuifuata ili kuufikia utukufu: ni sauti ya Yesu. Tukio hili linatupa matumaini kwamba mateso na msalaba si mwisho wa safari yetu ya kiroho, bali njia ya kuufikia utukufu kwa njia ya ufufuko. Tumwombe Mungu neema itakayotuwezesha kung’ara kiroho ili nasi hatimaye siku moja tupate kuingia katika utukufu wa Mungu. SALA: Ee Yesu utujalie nasi tuushiriki utukufu wako. |