Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 10/08/2024
2024 AGOSTI 10: JUMAMOSI-JUMA LA 18 LA MWAKA
MT. LAURENTI, SHEMASI NA SHAHIDI
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Juma II
Somo 1. 2 Kor 9:6-10
Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna sikuzote, mpate kuzidi sana katika tendo jema; kama ilivyoandikwa, ametapanya, amewapa maskini, haki yake yakaa milele. Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu. |
Wimbo wa Katikati. Zab 112:1-2, 5-9
1. Heri mtu yule amchaye Bwana, (K) Heri atendaye fadhili na kukopesha. 2. Nuru huwazukia wenye adili gizani; 3. Amekirimu, na kuwapa masikini, |
Injili. Yn. 12:24-26
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu. |
TAFAKARI
TUJITOE KIKAMILIFU KATIKA UTUME WA KRISTO: Tunaadhimisha sikukuu ya Mt. Laurenti, shemasi na shahidi. Meza ya neno la Mungu katika masomo yote yanatuhimiza kutambua kuwa maisha yetu ya hapa duniani ni kama mbegu, tunatakiwa tujitoe kama vile mkulima anavyootesha mbegu katika ardhi na kutarajia mavuno mengi baadaye. Mt. Laurenti alifanya hivyo, na leo tunaalikwa kutambua bado iko nafasi ya kujitoa sadaka ili kufanikisha maisha yetu ya mbinguni. Mwaliko ni kuwa kila mmoja wetu atende kama alivyokusudia. Tuwe tayari kujitosa katika utume wa familia, jumuiya, Kanisa na hata taifa kwa ujumla. Sadaka zetu zinahitajika. Wengi wetu bado ni waoga na hawajathubutu kujitosa kikamilifu katika huduma za Kanisa na jamii ili kuwafikia wahitaji. Mafanikio binafsi si mafanikio ya kweli. Majitoleo ndiyo yanayodaiwa na Mungu na Kanisa lake. Yesu alijitoa kuwa mbegu ya Kanisa na sasa tunayo matunda mengi. Mt. Laurenti alijitoa na leo tunamkumbuka kwa shangwe. Mimi na wewe leo tunaalikwa kufanya maazimio ya ufuasi na kujitoa kikamilifu. SALA: Ee Bwana utujalie roho ya Mt. Laurenti ili nasi tujitoe kwako bila ya kujibakiza. |