Masomo ya misa

Masomo ya Misa: Dominika ya 33

By

on

Rangi: Kijani
Zaburi: Juma I

SOMO 1. Dan 12: 1-3

Wakati ule Mikaeli atasimama, jemedari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile. Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele. 

WIMBO WA KATIKATI. Zab 16: 5, 8-11

“1. Bwana ndiye fungu la posho langu,
Wewe unaishika kura yangu.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.

(K) Mungu unihifadhi mimi, kwa maana nakukumbilia wewe.

  1. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
    Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
    Maana hutaiacha nafsi yangu kuzimu,
    Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. (K)
  2. Utanijulisha njia ya uzima,
    Mbele ya uso wako ziko furaha tele.
    Na katika mkono wako wa kuume,
    Mna mema ya milele. (K)”

SOMO 2. Ebr 10: 11- 14, 18

Kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu; tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanotakaswa. Basi, ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi. 

INJILI. Mk 13: 24-32

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Siku zile, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota za mbinguni zitakuwa zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. Ndipo atakapowatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu. Kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake liishapo kuwa laini, na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno ni karibu; nanyi kadhalika, myaonapo mambo hayo yanaanza, tambueni ya kuwa yu karibu milangoni. Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe. Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.

TAFAKARI

UTAVUNA ULICHOPANDA
Hakuna jambo lisilo na mwisho. Hata maisha yetu hapa duniani yatafikia mwisho wake. Kwa hakika siku hiyo itakuja, siku ambayo kila mmoja wetu ataitwa kutoa hesabu ya maisha yake wakati wa hukumu ya mwisho. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha yafuatayo kuhusiana na siku hiyo ya mwisho: “Ufufuko wa wafu, wote wenye haki na wasio haki, utaitangulia hukumu ya mwisho. Huu utakuwa ni wakati ambapo wote walio makaburini wataisikia sauti ya Mwana wa Adam nakuelekea kila mmoja, wale waliotenda mema katika ufufuko na wale waliotenda mabaya katika hukumu. Kisha Kristo atakuja katika utukufu wake akiambatana na malaika wote… Mataifa yote watakusanyika mbele yake, na atawatenganisha kila mmoja peke yake kama vile mchungaji anavyowatenganisha mbuzi na kondoo, na atawaweka kondoo upande wa kuume, bali mbuzi upande wa kushoto… na wataenda zao katika adhabu ya milele, lakini waadilifu katika uzima wa milele” (KKK 1038).
Masomo ya Dominika ya 33 ya mwaka B wa Kanisa hututafakarisha juu ya siku hiyo ya hukumu ya mwisho. Ni siku hii ambayo kila mmoja anao uhakika itafika, na tutahukumiwa kadiri ya matendo yetu. Siku hii kila mmoja atavuna kile alichopanda “wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele.” Katika somo la kwanza inaandikwa wazi kwamba “walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele.” Dominika kadhaa zilizopita tuliambiwa, kuwa na hekima ni kuwa na Mungu ndani yako na hivyo kuyaona yote kadiri ya jicho la Mungu. Hivyo ung’aavu huo wa siku ya mwisho unasababishwa na namna mmoja anavyojishibisha hekima ya Mungu kwa Neno lake na Sakramenti zake. Nyenzo hizi humpeleka mmoja kuwa karibu na Mungu, kujitegemeza kwake, kujifunza kutoka kwake na kutenda kadiri ya mapenzi yake Mungu. Na hii ndiyo njia ya kufikia uzima wa milele.
Njia ya pili ni kuwaongoza watu katika haki. Ni wajibu wa kimisionari wa kuwapeleka watu katika utakatifu. Huu ni wajibu wa kuwa mbele ya wengine kama ishara ya uwepo wa Mungu kwao. Dominika ya leo mama Kanisa pia anaadhimisha siku ya pili ya maskini duniani inayoongozwa na ujumbe ufuatao: “Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, akamwokoa na taabu zake zote” (Zab 34:6). Ni ujumbe ambao unaendana vema na jukumu hili la kuwaongoza watu katika haki. Kilio kikubwa kwa maskini ni kukosa haki. Baba Mtakatifu Fransisko anakumbusha katika ujumbe wake maalum kwa siku hii sababu za umaskini akisema: “Umaskini si jambo ambalo linatamaniwa na mtu yeyote, bali husababishwa na ubinafsi, majivuno, tamaa na kutotenda haki.” Kwa maneno mengine mmoja anaingia katika hali ya umaskini kwa sababu amefungiwa vioo na jirani yake na hakuna anayemsikia. Hivyo kilio chake ukipeleka kwa Mungu huku akijiachilia mikononi mwake mzima mzima akiwa na matumaini kwake kama Baba anayeweza kumsaidia na kumwelewa.
Katika ujumbe wake Baba Mtakatifu Fransisco anaelezea matendo matatu yaliyomo katika ujumbe huo ambayo yakitafakariwa vizuri huwa ni njia ya kuwafikia wengine hasa wanaoteseka katika hali umaskini katika haki. Tendo la kwanza ni kilio cha maskini. Baba Mtakatifu anakumbusha kilio cha maskini kwa namna mbalimbali. Ingawa kilio hiki anakipeleka kwa Mungu, lakini Mungu anahitaji mimi na wewe kuwa vyombo vya kusikiliza kilio hicho. Baba Mtakatifu anatuonya juu ya hatari ya sisi tunaopaswa kusikiliza kuacha kuwabeza au kuweka mipango na matarajio yetu au kuepuka kelele zao kama jambo linalohatarisha kupokonya usalama wetu. Namna hiyo hutuingiza katika hali ya kutokupata fursa ya kufikiwa na kilio cha maskini walio mbele yetu. Ni katika hali ya ukimya na unyenyekevu ndipo tunapata fursa ya kufikiwa na kilio cha maskini. Wajibu wetu wa kimisionari ni kukisikia kilio chao na kutoa jawabu litakalokidhi haja yao na si kufanya mikakati mbalimbali ambayo itazikidhi haja zetu tu.
Tendo la pili ni “kusikiliza.” Hii ni hali ya kuipatia nafasi sauti ya mwenye kiu ya haki. Kama tulivyotafakari Dominika mbili zilizopita tulimwona Kristo akionesha usikivu huo wa Mungu katika uponyaji wa Bartimayo mwana Timayo aliyekuwa kipofu. Kwa waliokuwa pembeni wakiambatana na Kristo kipofu huyo alikuwa kero na hakuna aliyekipatia kilio chake nafasi. Ila Kristo aliye ufunuo wa Upendo wa Mungu alimpatia nafasi na kumsikiliza kilio chake: “unataka nikufanyie nini?” Pengine wengine walidhani alitaka tu kuomba msaada wa pesa au chakula au mahitaji mengine ya watu waliopatwa na madhila kama yake. Lakini Kristo hakufanya hivyo bali alimpatia nafasi na kutaka kusikiliza hamu ya moyo wake. “Mwalimu wangu, nataka nipate kuona”. Mara ngapi hatusikilizi kiu ya maskini anayetujia na hivyo kufanya yale tunayofikiri na kuyataka sisi? Inatugharimu nini kujishusha na kuisikiliza kiu ya haki aliyonayo mmoja anayekujia na hivyo kujibu kiu hiyo sawasawa?
Tendo la tatu ni “kuokoa.” Kilio cha maskini kwa Mungu ni kurudishiwa kilichopokonywa au kuondolewa kwake. Uovu katika tafsiri yake makini huelezewa kama upungufu wa ukamilifu. Tendo la Kristo kuja ulimwenguni lilinuia katika kumuokoa mwanadamu na kumrudishia haki yake mbele ya Mungu. Mungu anaahidi na kutenda. Kilio cha maskini kwake kinapitia katika masikio yetu na hivyo tunategemewa sisi kuwafikisha hawa wanaopungukiwa katika haki ya Mungu. Namna hii ya kumuokoa maskini inaonekana katika namna mbalimbali kadiri ya aina ya kilio na mahali kinaposikika kilio hicho. Kilio cha maskini kinatugutusha katika muunganiko wetu wa kindugu na kwamba mmoja asijisikie furaha na kukamilika wakati mwenzake jirani yake amepungukiwa. Kama nilivyoeleza hapo mwanzo kuwa hakuna anayependa kuwa maskini lakini umaskini hutokana na ubinafsi wetu na kutokupenda haki.
Katika Injili Kristo anatupatia hekima ya juu kabisa. Kwanza anathibitisha ujio wa siku hiyo ya mwisho na kisha anaeleza wazi kuwa “hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.” Maneno ya Kristo yanathibitisha uaguzi wa Nabii Danieli katika somo la kwanza. Siku ya mwisho itafika na Mwana wa Adamu “atawatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu.” Lakini siku hii itakuja lini hakuna anayejua. Hapa ndipo penye hekima ya Kristo ambayo inatuelekeza si katika kuifikiria siku hiyo wakati itakapokuja au namna itakavyokuja bali ni namna utakavyokutwa. Ni suala la kujiuliza kama kweli utakuwepo katika orodha ya wateule wa Mwana wa Adamu. Sifa zile mbili za somo la kwanza zinajirudia, yaani kuwa na hekima na kuwaongoza wengine katika haki. Sifa hizi zinatuonesha zaidi tulivyomtukuza Mungu kwa matendo mema kwa wenzetu; zinatuonesha jinsi tuivyokuwa ufunuo wa Mungu kwa wenzetu. Kwa maneno mengine Kristo anatumbusha kuzaa matunda ya imani kadiri ya Neno lake kusudi siku hiyo itakapofika ikufanye wewe na mimi kuwa miongoni mwa wateule wake.
Sadaka ya Kristo msalabani imetutakasa wote na kutuunganisha na Mungu. Kwa tendo lake hili la upendo ametufanya sisi kuwa watoto wa Mungu. “Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu; tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake.” Sadaka hii ni uthibitisho wa usikivu wa Mungu kwa kilio cha mwanadamu aliyekuwa amegalazwa na dhambi. Sadaka hii ikatufanya sisi tuliokuwa mwanzo adui kwa sababu ya dhambi kuwa tena rafiki za Mungu. Sadaka hii imetuunganisha na Mungu. 

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2025 2024 2023 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you