Terence Crawford Afungua Njia kwa Mabondia wa Tanzania, Mamia Wajitokeza DUNDA
Mamia ya mabondia kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania wamejitokeza kuwania nafasi ya kushiriki Ligi ya DUNDA Tanzania Semi Pro, iliyoanzishwa kwa ushiriki wa bingwa wa dunia wa ngumi kutoka Marekani, Terence “Bud” Crawford.
Crawford, ambaye ameshinda mapambano yote 41 aliyopigana katika ngumi za kulipwa, alishiriki uzinduzi wa ligi hiyo tarehe 25 Mei 2026 katika Ufukwe wa Coco, Dar es Salaam. Bondia huyo, ambaye amewahi kuwa bingwa wa dunia katika madaraja tofauti ya uzito, ataendelea kuwa Mshauri na Balozi wa DUNDA katika ngazi ya kimataifa.
Ligi hiyo ni ya kwanza ya ngumi za nusu kulipwa nchini Tanzania, ikiandaliwa na kuendeshwa kwa ubia kati ya Times FM na Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC).
Katika hatua ya kuelekea kuanza kwa mashindano, DUNDA iliendesha mchujo wa mabondia tarehe 3 na 4 Oktoba 2026 katika eneo la Maegesho ya Wavuvi, Coco Beach, Dar es Salaam.
Mabondia walijitokeza kwa wingi kuanzia asubuhi hadi jioni, wakionyesha uwezo wao mbele ya majaji wenye uzoefu katika mchezo wa ngumi. Mchujo huo ulifanyika kwa ushirikiano na TPBRC.
DUNDA inalenga kuwapa mabondia wanaochipukia nafasi ya kupigana mara kwa mara, kupata uzoefu, kujenga rekodi zao na kujiandaa kuingia kwenye ngumi za kulipwa.
Kwa mabondia wenye ndoto ya kufika mbali, ligi hiyo inatoa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao na kujenga majina yatakayowasaidia kupata fursa zaidi ndani na nje ya Tanzania. Pia inalenga kuwasaidia kutumia mchezo wa ngumi kama njia ya kujipatia kipato katika siku zijazo.
Ushiriki wa Crawford katika DUNDA unatarajiwa kusaidia kukuza vipaji vya mabondia wa Tanzania na maendeleo ya ligi hiyo.
Baada ya mchujo kukamilika, hatua inayofuata ni kuwachunguza na kuwathibitisha mabondia wanaokidhi vigezo vya kushiriki mashindano. Zoezi hilo litafanyika kwa ushiriki wa TPBRC.
Mabondia watakaokidhi vigezo watafanyiwa vipimo rasmi vya uzito na uchunguzi wa afya kabla ya kupangwa kwa mapambano.
Mwezi Novemba 2026, DUNDA inatarajia kutangaza majina ya mabondia waliochaguliwa kushiriki msimu wa kwanza, mfumo wa mashindano, ratiba ya mapambano na zawadi zitakazotolewa kwa mabingwa.
Kwa mwitikio mkubwa ulioonekana wakati wa mchujo, ligi hiyo sasa inaelekea kwenye hatua ya kuanza mashindano yake ya kwanza, huku matarajio yakiwa ni kuona mabondia wapya wakipata nafasi ya kuonyesha uwezo wao na kuendeleza ndoto zao za kufika kwenye ngumi za kulipwa.




