Masomo ya misa

Masomo ya Misa Oktoba 31

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 31/10/2024

2024 OKTOBA 31: ALHAMISI: JUMA LA 30 LA MWAKA

Mt. Alfonsi Rodriges, Mtawa
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma II

SOMO 1. Efe 6: 10-20

Mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya Yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili, ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika hiyo kunena jinsi inipasavyo kunena.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 144: 1-2, 9-10

1. Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu,
Anifundishaye mikono yangu vita,
Vidole vya kupigana.

(K) Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu.

2. Mhisani wangu na boma langu,
Ngome yangu na mwokozi wangu,
Ngao yangu niliyemkimbilia,
Huwatiisha watu wangu chini yangu. (K)

3. Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya,
Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia.
Awapaye wafalme wokovu,
Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu. (K)

INJILI. Lk 13:31-35

Siku moja, Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea Yesu, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu. Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka. Angalieni, mmeachiwa nyumba yenu! Nami nawaambia, Hamtaniona tena kamwe, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.

TAFAKARI

KWA MATAKWA YA MUNGU: “Siku moja, Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea Yesu, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua.” Mara kwa mara inatokea kwamba katika maisha, mambo yanatokea kwa bahati mbaya, kwa maamuzi ya mtu fulani, au kwa bahati nzuri. Yesu alijua wazi kwamba maisha yanakuwa yalivyo kutokana na mpango wa Mungu. Herode angeweza kumwinda lakini maisha yake yapo katika mikono ya Mungu. Vivyo hivyo kwako wewe na mimi. Usihofu vitisho, ajali au uovu. Maisha yetu yameshikiliwa na Mungu. Usihofu utafikia malengo ambayo Mungu amekuwekea. Yesu alihuzunishwa na kitendo cha Waisraeli kuukataa ujumbe wa Mungu. Huruma yake kwa watu ni matokeo ya upendo mkubwa alionao. Nawe pia unapaswa kuwa hivyo. Upendo unapong’aa, uache ung’ae. Upendo unapolia usiufiche. Yesu alizungumzia wazi wazi hisia zake, alisema wazi sababu ya huzuni yake. Tumfuate na kufanya vivyo hivyo.

SALA: Ee Mungu, tunakushukuru kwa sababu maisha yetu yapo mikononi mwako.

The post Masomo ya Misa Oktoba 31 appeared first on CLARETIAN PUBLICATIONS-EAST AFRICA.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2025 2024 2023 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you