Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 11/10/2024
2024 OKTOBA 11: IJUMAA-JUMA LA 27 LA MWAKA
Mt. Yohane wa XXIII, Papa
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma III
SOMO 1. Gal 3:7-14
Fahamuni basi, yakuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa. Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani. Kwa maana wale walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye. Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani. |
WIMBO WA KATIKATI. Zab 111:1-6
1. Aleluya. (K) Alikumbuka agano lake milele. 2. Kazi yake ni heshima na adhama, 3. Amewapa wamchao chakula, |
INJILI. Lk 11:15-26
Wengine wa makutano walisema, “Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo.” Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia, “Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli. Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je, huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake. Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutawanya. “Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, ‘Nitarudia nyumba yangu niliyotoka.’ Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.” |
TAFAKARI
KUVUKA MSTARI: Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. Katika filamu ‘Hook’ kijana Peter Pan alichora mstari mchangani, kisha akawaambia kila mtu anayeamini na avuke huo mstari. Peter alisahau kwamba wako wanaoweza kuamua asivuke mstari badala yake akasimama katikati ya mstari (hayuko upande wowote). Ikiwa tunamwamini Yesu kuwa Bwana na Mwokozi, tunapaswa kuyapima mambo, kutafuta uwezekano, kufanya maamuzi, kuvuka mstari, na kumtumainia Mungu. Inawezekana tumekuwa na changamoto nyingi katika maisha, inawezekana tumekuwa na maswali ambayo hayajajibiwa bado, hilo lisitukatishe tamaa, sio kwamba hatuna maana au thamani mbele za Mungu, maswali yetu yana maana na ni ya muhimu. Tafuteni nanyi mtaona; Mashaka tuliyonayo kuhusu imani yatamalizika. Bisheni nanyi mtafunguliwa. Mahitaji uliyonayo ni ya muhimu. Ombeni nanyi mtapewa; tudumu katika sala. SALA: Bwana utujalie kuyapima mambo ya ulimwengu huu ili tujipatie busara. |