Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Oktoba 29

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 29/10/2024

2024 OKTOBA 29: JUMANNE: JUMA LA 30 LA MWAKA

Mwenyeheri Maria Resituta
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma II

SOMO 1. Efe 5:21-33

Hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo. Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lolote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa. Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 128:1-5

1. Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika njia yake.
Taabu ya mikono yako hakika utaila;
Utakuwa heri, na kwako kwema.

(K) Heri kila mtu amchaye Bwana.

2. Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
Nyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni
Wakiizunguka meza yako. (K)

3. Tazama, atabarikiwa hivyo, Yule amchaye Bwana.
Bwana atakubariki toka Sayuni;
Uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako. (K)   

INJILI. Lk 13:18-21

Yesu alisema, “Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini? Umefanana na punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake.” Akasema mara ya pili, “Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia.”

TAFAKARI.

OTESHA MAISHA: Ufalme wa Mungu umefanana na punje ya haradali aliyoitwaa mtu akaitupa katika shamba lake. Kuna uwezekano mkubwa kwamba hujawahi kupanda mbegu ya haradali, wala kuiona ikiota. Usipime ukubwa wa mti ukilinganisha na mbegu yake. Kipindi kijacho cha masika chukua mbegu tena zile zilizo ndogo. Mbegu hiyo inawakilisha maisha yako na Mungu. Ioteshe mbegu hiyo. Itunze kwa kuimwagilia maji na kuitilia samadi au mbolea. Kila mara unapokwenda kuitazama hiyo mbegu, mtukuze Mungu kwa imani yako inayoendelea kukua. Mbegu hiyo inawezekana inakua taratibu na katika ukimya, lakini inachanua, inakua na kuzaa. Unapomwagilia mmea wako mwagilia pia na moyo wako kwa Neno la Mungu (yasome Maandiko Matakatifu kila siku). Unapopalilia ondoa pia shughuli zote zinazofanya hali yako ya kiroho kudumaa. Unapoutazama ukichanua, mshukuru Mungu kwa ajili ya upendo wake mkuu kwako.

SALA: Bwana Yesu utujalie imani yetu ndogo na dhaifu ikuzwe na neema zako ili matendo yapate kuzaa matunda.

The post Masomo ya Misa Oktoba 29 appeared first on CLARETIAN PUBLICATIONS-EAST AFRICA.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2023, 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you