Masomo ya misa

Masomo ya Misa Oktoba 25

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 25/10/2024

2024 OKTOBA 25: IJUMAA: JUMA LA 29 LA MWAKA

Mt. Magareta Klithero, Mfiadini
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma I

SOMO 1. Efe 4:1-6

Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 24:1-6

1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.

(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.

2. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili,
Wala hakuapa kwa hila. (K)

3. Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)

INJILI. Lk 12:54-59

Yesu aliwaambia makutano pia, “Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, ‘Mvua inakuja;’ ikawa hivyo. Na kila ivumapo kaskazi, husema, ‘Kutakuwa na joto;’ na ndivyo ilivyo. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya? “Na mbona ninyi wenyewe kwa nafsi zenu hamwamui yaliyo haki? Maana, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidii kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi; yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani. Nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.”

TAFAKARI

TUMEITWA: Mungu ametuchagua ili tumwakilishe Kristo hapa duniani. Katika mwanga wa ukweli wake, tunapaswa kuishi kulingana na wito huo tulioupokea. Tumepata upendeleo wa kuchaguliwa kuwa watu wake. Hili linajumuisha kuwa wapole, wanyenyekevu, wavumilivu, waelewa, na watu wa amani. Watu wanayatizama maisha yetu. Je! Wanamwona Kristo ndani yetu? Ni kwa kiasi gani tunamwakilisha? Pengine fadhila nyingine ambazo tunapaswa kuwa nazo ni ngeni katika jamii zetu. Mfano fadhila hii ya uvumilivu. Je, Umewahi kuvuka mbio barabara wakati magari yakienda kwa kasi eti kwa sababu una haraka? Je! unateseka na changamoto hii ya kukosa uvumilivu katika sehemu nyingine tofauti na hizo tulizotaja? Kama jibu ni hapana basi jiambie mwenyewe kwamba umeshindwa kwa sababu wewe ni mwongo. Tunaishi katika ulimwengu unaotaka mambo ya papo kwa hapo, na tunategemea matokeo ya papo kwa hapo. Paulo anatutaka tuvumiliane. Tuanze kwa kutafakari jinsi Mungu alivyo mvumilivu kwetu na turuhusu neema hiyo ya Mungu itiririke ndani mwetu.

SALA: Ee Mungu unayetuvumilia licha ya mapungufu yetu, utujalie moyo wa kuwavumilia wenzetu katika mapungufu yao.

The post Masomo ya Misa Oktoba 25 appeared first on CLARETIAN PUBLICATIONS-EAST AFRICA.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2025 2024 2023 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you