Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 30/05/2024
2024 MEI 30 : ALHAMISI-JUMA LA 8 LA MWAKA
Mt. Yohana wa Arki, Bikira
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 3
Somo 1. 1 Pet 2: 2-5. 9-12
Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ikiwa mmeonja ya kwamba Bwana ni mwenye fadhili. Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo. Ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema. Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. Mwe na mwenendo mzuri katika ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa. |
Wimbo wa Katikati. Zab 100: 2-5
1. Mtumikieni Bwana kwa furaha; (K)Njoni mbele za Bwana kwa kuimba kwa furaha. 2. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu; 3. Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru; 4. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema; |
Injili. Mk 10: 46-52
Walifika Yeriko; Yesu alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka anakuita. Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani. |
TAFAKARI
IMANI INAPONYA: Katika Injili ya leo tumesikia jinsi imani ilivyomponya kipofu Bartimayo. Kabla ya kuponywa kipofu huyu alikumbana na kikwazo kutoka kwa wale waliokuwa wanaongozana na Yesu kujaribu kumzuia. Bartimayo alitumia fursa ya imani aliyokuwa nayo na sauti yake kuomba msaada kwa Yesu ili asimpite bali amponye na kwa imani yake alipata uponyaji aliotamani. Tujifunze kuwa nasi tuna upofu fulani hata kama siyo upofu wa kutoona kwa macho ya nyama inaweza kuwa tuna upofu wa kutoona mahitaji ya wengine labda kutokana na mapungufu yetu. Kwa imani na matumaini tupaaze sauti zetu tumwombe Yesu asitupite bali atuponye. Tunafundishwa kuwa katika safari yetu ya kutafuta wokovu tusikate tama. Tunaweza kukatishwa tamaa hata na wale tunaoishi nao. Wahenga walisema “Kikulacho ki nguoni mwako.” Wale waliokuwa wanamfahamu Bartimayo na shida yake ndiyo hao hao waliokuwa wa kwanza kumzuia asikutane na Yesu. Rafiki zetu, ndugu zetu na jamaa zetu wanaweza kuwa kikwazo kwetu kufikia wokovu ila tushinde vikwazo hivyo kwa imani. Sala: Ee Yesu tunaomba utujalie fadhila ya kuomba kwa imani.
|