Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Juni 19

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 19/06/2024

2024 JUNI 19 : JUMATANO-JUMA LA 11 LA MWAKA

Mt. Romuald, Abate
Rangi: Kiani
Zaburi: Juma 3

Somo 1. 2 Fal 2:1, 6-14

Bwana alipopenda kumpandisha Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya alitoka Gilgali pamoja na Elisha. Eliya akamwambia, “Tafadhali kaa hapa; maana Bwana amenituma niende mpaka Yordani.” Akasema, “kama Bwana aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha.” Wakaendelea mbele wote wawili.  Basi watu hamsini wa wale wana wa manabii wakaenda wakasimama, kuwakabili kwa mbali; na hao wawili wakasimama karibu na Yordani. Eliya akalitwaa vazi lake la juu, akalikunja, akayapiga maji, yakagawanyika huku na huku, na hao wawili wakavuka pakavu. Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, “Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako.” Elisha akasema, “Nakuomba, sehemu mara dufu ya roho yako iwe juu yangu.” Akasema, “Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la, hukuniona, hulipati.” Ikawa walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, “Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake!” Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili. Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, “Yuko wapi Bwana, Mungu wa Eliya?” Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huko na huko, Elisha akavuka.

Wimbo wa Katikati. Zab 31:20, 21-24

1.  Jinsi zilivyo nyingi Fadhili zako
Ulizowawekea wakuchao;
Ulizowatendea wakukimbiliao
Mbele ya wanadamu!

(K) “Iweni hodari, mpige moyo konde,
ninyi nyote mnaomngoja Bwana.”

2. Utawasitiri na fitina za watu
Katika sitara ya kuwapo kwako. (K)

3. Mpendeni Bwana,
Ninyi nyote mlio watauwa wake.
Bwana huwaifadhi waaminifu,
Humlipa atendaye kiburi malipo tele. (K)

Injili. Mt 6:1-6, 16-18

Yesu aliwaambia wanafunzi wake; “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. “Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu.  Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao.  Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao; ili waonekane na watu kuwa wanafunga, Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.”

 

 

TAFAKARI

WEMA UNAJITANGAZA WENYEWE: Injili ya leo inatualika tutafakari kuhusu misaada mbalimbali tunayotoa kwa wahitaji, maisha ya sala na kufunga. Matendo haya yanakuza maisha yetu ya kiroho pale yanapotendeka katika roho ya Injili. Yesu anatupa tahadhari ili tusifanye wema kwa lengo la kuonekana na kusifiwa bali tutende wema kwani unahitajika. Katika jamii zetu kuna watu au taasisi na mashirika mbalimbali ambao wakitoa msaada fulani ni lazima Taifa lote lifahamu kwani misaada hiyo husindikizwa na vyombo mbalimbali vya habari iweze kuonekana kila mahali. Leo Yesu anatualika tuwe tayari kutoa misaada hii pasipo kujionesha kwani Mungu anayetusukuma kutenda wema huo, anaona moyo wa mtoaji na haitaji vyombo vya habari ili aweze kuona. Yesu anatufundisha pia kuwa sala nzuri ni ile inayotoka moyoni na siyo ya kujionesha. Si lazima wakati wa sala kuweka vipaaza sauti vikubwa ili watu watambue tunasali. Mungu hahitaji tujioneshe kwa watu kwani hata kabla ya kusali yeye anajua.

SALA: Ee Yesu nijalie moyo wa sala katika unyekekevu.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2023, 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you