Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 03/07/2024
2024 JULAI 3: JUMATANO; JUMA LA 13 LA MWAKA
MT. TOMA, MTUME
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Tazama Sala ya Siku
Somo 1. Efe 2:19-22
Tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho. |
Wimbo wa Katikati. Zab 117
1. Aleluya. (K) Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili. 2. Maana Fadhili zake kwetu sisi ni kuu, |
Injili. Yn 20:24-29
Mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. Basi wanafunzi wengine wakamwambia,”Tumemwona Bwana.” Akawaambia, “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo.” Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema,”Amani iwe kwenu.” Kisha akamwambia Tomaso, “Lete hapa kidole chako, uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.” Tomaso akajibu, akamwambia,” Bwana wangu na Mungu wangu!” Yesu akamwambia,” Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.” |
TAFAKARI.
BWANA WANGU NA MUNGU WANGU: Haya ni maneno ya kukiri imani aliyotamka Mtume Toma baada ya kuishi katika mashaka kwa muda mrefu tangu Kristo alipokamatwa, akateswa, akafa na akafufuka. Toma anapokutana na Kristo Mfufuka akajidhihirisha kwake kwa kuona bayana madonda yake hakusita kuamini. Toma anabadilika kutoka mwelekeo wake wa mashaka, wasiwasi na imani haba, anaamini. Kristo anawasifu zaidi wanaosadiki bila kuona. Kwa maisha ya mtume huyu twakumbushwa kuwa imani ni kuwa na uthabiti katika vitu tunavyotumaini, na hakika ya mambo yasiyoonekana. Ndio huo msimamo Paulo anaowakumbushia Waefeso kuwa kwa imani wamekuwa ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mwenye imani anajisikia nyumbani, nyumbani humu haishi kwa wasiwasi, au mashaka bali akitambua kuwa amefanyika mtoto wa Mungu na wa Kanisa kwa Sakramenti ya Ubatizo. Tutambuapo hivyo tutajibidiisha kustawi katika wema kama Mtakatifu Toma na tutakuwa majasiri wa kutosha kusema pamoja naye “twende na tufe pamoja na Yesu.” Sala: Kwa maombezi ya Mtakatifu Toma, Ee Bwana tuwezeshe kuondoa mashaka yote na kukuamini daima. |