Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 21/07/2024
2024 JULAI 21: DOMINIKA YA 16 YA MWAKA
Rangi: Kijani
Zaburi: Tazama Sala ya Siku
Somo 1. Yer 23: 1-6
Ole wao wachungaji, wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya! asema Bwana. Kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, juu ya wachungaji wanaowalisha watu wangu, mmetawanya kundi langu, na kuwafukuza, wala hamkwenda kuwatazama; angalieni, nitawapatiliza uovu wa matendo yenu, asema Bwana. Nami nitakusanya mabaki ya kundi langu, katika nchi zile zote nilizowafukuza, nami nitawaleta tena mazizini mwao; nao watazaa na kuongezeka. Nami nitaweka juu yao wachungaji watakaowalisha; wala hawataona hofu tena, wala kufadhaika, wala hatapotea hata mmoja wao, asema Bwana. Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi. Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama; na jina lake atakaloitwa ni hili Bwana ni haki yetu. |
Wimbo wa Katikati. Zab 23:1-6
1. Bwana ndiye mchungaji wangu, (K) Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. 2. Huniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake, 3. Waandaa meza mbele yangu, 4. Hakika wema na fadhili zitanifuata |
Somo 2. Efe 2: 13-18
Katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani. Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba. Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu. Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja. |
Injili. Mk 6: 30-34
Mitume walikusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya na mambo yote waliyoyafundisha. Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha; mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu. Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika. Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi. |
TAFAKARI
BIDII KATIKA UTUME SALA: Ee Bwana Yesu tunakuomba utujalie moyo wa toba. |