Jumanne: Juma la II la Majilio
Kumbukumbu ya Hiyari
Rangi: Urujuani
Zaburi: Juma II
SOMO 1. Isa 40:1-11
Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo watu wangu, asema Mungu wenu. Semeni na moyo wa Yerusalemu, kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa; kwa kuwa amepokea kwa mkono wa Bwana adhabu maradufu kwa dhambi zake zote. Sikilizeni, ni sauti ya mtu aliaye, itengenezeni nyikani njia ya Bwana; nyoosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu. Kila bonde litainuliwa, na kila mlima na kilima kitashushwa; palipopotoka patakuwa pamenyoka, na palipoparuza patasawazishwa; na utukufu wa Bwana utafunuliwa, na wote wenye mwili watauona pamoja; kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya. Sikiliza, ni sauti ya mtu asemaye, Lia! Nikasema, nilie nini? Wote wenye mwili ni majani, na wema wake wote ni kama ua la kondeni; majani yakauka, ua lanyauka; kwa sababu pumzi ya Bwana yapita juu yake. Yakini watu hawa ni majani. Majani yakauka, ua lanyauka; bali neno la Mungu wetu litasimama milele. Wewe uhubiriye Sayuni habari njema, panda juu ya mlima mrefu; wewe uhubiriye Yerusalemu habari njema, paza sauti kwa nguvu, paza sauti yako, usiogope; iambie miji ya Yuda, Tazameni Mungu wenu. Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa, na mkono wake ndio utakaomtawalia; tazameni, thawabu yake i pamoja naye, na ijara yake i mbele zake. Atalilisha kundi lake kama mchungaji, atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake; na kuwachukua kifuani mwake, nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.
WIMBO WA KATIKATI. Zab 96:1-3, 10-13
“1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana libarikini jina lake,
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
(K) Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa.
- Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake.
Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki,
Atawahukumu watu kwa adili. (K) - Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo.
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha. (K) - Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi,
Atahukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake. (K) “
INJILI. Mt 18:12-14
Siku ile, Yesu aliwaambia wafuasi wake. Mwaonaje? mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! hawaachi wale tisa na tisini, akaenda milimani, na kumtafuta yule aliyepotea? Hata akipata kumwona, amin, nawaambia, amfurahia huyo zaidi, kuliko wale tisa na tisini wasiopotea. Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.
TAFAKARI
UTUME WA KUWATAFUTA: Makanisa mengi ulimwenguni kote yameanza kugundua mbinu na njia zitakazokubalika na wale wasio waamini. Wengine wameanzisha utume wa kutoka na kwenda kuwatafuta waamini wapya, wakiwapelekea Habari njema wale walioachwa, mashoga na wale waliotupwa au kuachwa na makanisa yao. Mara nyingi makanisa haya yanakutana na mapingamizi, na kulaumiwa na makanisa mengine kwa kusahau kazi ya kulichunga kundi. Kwa nguvu na maweza yetu yote, kwa ubunifu na kwa njia mbali mbali, tunapaswa kwenda na kuwatafuta wale waliopotea, waliomwacha Mungu. Tunapaswa kuwa wachungaji tunaowatafuta walio wageni na wanaotangatanga. Yeye mwenyewe, aliwaacha wale tisa na tisini na kwenda kumtafuta yule mmoja aliyepotea hata amwone. Tulisaidie kanisa kutafuta njia bora na za kufaa katika kuchukua ujumbe wa injili na kuwafikia watu wote wanaotuzunguka hasa wale wasioamini.
SALA: Ee Mungu utujalie hamu ya kuwatafuta wale waliopotea au kujitenga nawe na kuwarudisha kwako.