Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Alhamisi ya Pasaka

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 04/04/2024

2024 APRILI 4 : ALHAMISI-JUMA LA KWANZA LA PASAKA

Mt. Isidori, Askofu na Mwalimu
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

Somo 1. Mdo 3:11-26

Siku zile, kiwete yule aliyeponywa alipokuwa akiwashika Petro na Yohane, watu wote wakawakusanyikia mbio katika tao lile lililoitwa tao la Sulemani, wakishangaa sana. Hata Petro alipoyaona haya akawajibu wale watu, Enyi Waisraeli, mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia macho sisi, kana kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi, au kwa utauwa wetu sisi? Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu; ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake. Na kwa imani katika jina lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua; na imani ile iliyo kwake yeye ilimpatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu ninyi nyote. Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda. Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani; ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu. Kwa maana Musa kweli alisema ya kwamba, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye katika mambo yote atakayonena nanyi. Na itakuwa ya kwamba kila mtu asiyemsikiliza nabii huyo ataangamizwa na kutengwa na watu wake. Naam, na manabii wote tangu Samweli na wale waliokuja baada yake, wote walionena, walihubiri habari za siku hizi. Ninyi mmekuwa watoto wa manabii na wa maagano yale, ambayo Mungu aliagana na baba zenu, akimwambia Ibrahimu, Katika uzao wako kabila zote za ulimwengu zitabarikiwa. Mungu, akiisha kumfufua mtumishi wake Yesu, alimtuma kwenu ninyi kwanza, ili kuwabarikia kwa kumwepusha kila mmoja wenu na maovu yake.

Wimbo wa Katikati. Zab 8:2ab, 5 -9

“1. Wewe, Mungu, Bwana wetu,
Jinsi lilivyotukufu jina lako duniani mwote;
Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
Na binadamu hata umwangalie? (K)

“Ee, Mungu, Bwana wetu;
jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote. “

2. Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima;
Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako.
Umevitia vitu vyote chini ya miguu yako. (K)

3. Kondoo, na ng’ombe wote pia;
Naam, na wanyama wa kondeni.
Ndege wa angani, na samaki wa baharini;
Na kila kipitiacho njia za bahari. (K) “

Injili. Lk 24:35-48

Wanafunzi waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate. Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu. Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho. Akawaambia, Mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo. Na baada ya kusema hayo aliwaonesha mikono yake na miguu yake. Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajbu, aliwaambia, Mna chakula cho chote? Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akala mbele yao. Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa ningali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii, na Zaburi. Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.

TAFAKARI

MUNGU ANATENDA: Katika somo la kwanza Petro aliwaeleza wazi watu kuwa si kwa uwezo wake yule kiwete aliweza kutembea, bali kwa uwezo utokao juu (Yesu). Watu walidhani ni Petro katenda hayo ili wamtukuze. Kuna watu katika jamii wana tabia ya kupenda kusifiwa hasa baada ya kutenda jambo fulani, wanapenda kuwa miungu watu, kupenda kuitwa majina ya sifa. Kupenda kuheshimiwa n.k. Leo Petro anatuangalisha tusipende hayo ya kidunia, tueleze ukweli kuwa ni Mungu anatenda. Katika Injili tumeona wale wafuasi wa Emau baada ya Yesu kujidhihirisha kwao waliona ni vizuri wawashirikishe na wenzao. Hili lilikuwa jambo jema na Yesu anajitokeza papo hapo. Wafausi wa Emau wanakuwa wajumbe wa furaha ya ufufuko. Yesu anatokea miongoni mwa wafuasi wake ili kuithibitisha furaha hiyo na kushiriki pamoja nao kwa kuwaondolea hofu na kuwajaza amani. Nasi pia tunaalikwa kuwa wajumbe wa furaha na amani ya Kipasaka kwa wenzetu.

SALA: Ee Kristo Mfufuka utujalie paji la amani.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2023, 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you