Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 30/08/2024
2024 AGOSTI 30: IJUMAA-JUMA LA 21 LA MWAKA
Mt. Pamakio
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 1
Somo 1. 1 Kor 1:17-25
Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika. Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, na akili zao wenye akili nitazikataa. Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mleta hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu? Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuzi wa lile neno linalohubiriwa. Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu. Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wa wanadamu. |
Wimbo wa Katikati. Zab 33:1-2, 4-5, 10-11
1. Mpigieni Bwana vigeregere, enyi wenye haki, (K) Bwana anajaza nchi na fadhili zake. 2. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili, 3. Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa, |
Injili. Mt 25:1-13
Yesu aliwaambia wafuasi wake: “Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara. Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, ‘Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.’ Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao. Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, ‘Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.’ Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, ‘Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.’ Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa. Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, ‘Bwana, Bwana, utufungulie.’ Akajibu akasema, ‘Amin, nawaambia, siwajui ninyi.’ Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa. |
TAFAKARI
TUTAFUTE HEKIMA YA MUNGU KATIKA UTENDAJI: Mtume Paulo akiendelea kuilea kiimani jumuiya ya Wakorintho, leo anatuonesha utendaji wa Mungu ulivyojaa hekima na uwezo. Utendaji wake unaruhusu mwanadamu ajiinue na kuonekana kama anapata ushindi, ila mwishowe mambo huwa kinyume kabisa. Nguvu yake imewawezesha waliojiaminisha kwake kutenda kwa umahiri mkubwa, ila wale waliojiinua mbele yake wameshangazwa na utendaji huo. Ili kunufaika na nguvu ya Mungu sharti tutafute uwezo na hekima yake. Yesu katika Injili ya leo anaonesha kwa wazi jinsi tofauti iliyopo kati ya hekima ya Mungu na ya kibinadamu. Watendaji wamegawanyika katika makundi mawili, lile linalowakilisha utendaji dhaifu wa kibinadamu na wale wanaotenda wakitegemea neema na hekima ya Mungu. Taa isiyoweza kutoa mwanga sehemu yenye giza, haina maana yoyote. Kutembea na roho zetu wakati hazina neema ya Mungu, hazikubali mpango wake ni sawa na kuwa na taa isiyoangaza wakati tunaendea giza. Waliotegemea neema ya Mungu wamejiwekea hazina ya kuhakikisha taa inawaka. SALA: Ee Bwana Yesu utujalie neema ili taa zetu ziendelee kuwaka siku zote. |