Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 10/10/2024
2024 OKTOBA 10: ALHAMISI-JUMA LA 27 LA MWAKA
Mt. Daniel Komboni, Askofu Mmisionari
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma III
SOMO 1. Gal 3:1-5
Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa? Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili? Mmepatikana na mateso makubwa namna hii bure? Ikiwa ni bure kweli. Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? |
WIMBO WA KATIKATI. Lk 1: 69- 75
1. Ametusimamishia pembe ya wokovu (K) “Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, 2. Tuokolewe na adui zetu 3. Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu |
INJILI. Lk 11:5-13
Yesu aliwaambia wafuasi wake: “Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, ‘Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu, kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake;’ na yule wa ndani amjibu akisema, ‘Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe?’ Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake. Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” |
TAFAKARI
TUSALI KWA IMANI: Yesu anatutia moyo kudumu katika sala. Sala inasaidia kuwatofautisha wale wasiosali na wale wanaosali. Kumeibuka wimbi la watu wanaotuma ujumbe katika mtindo wa sala na kuwataka watu wengine watume kwa watu kadhaa au katika makundi kadhaa kisha wataona muujiza. Mara nyingi ujumbe huo huendana na vitisho kwa yoyote atakayepuuzia. Kumbe sala haiwafanyi waamini wawe walegevu katika kufanya kazi waseme tu amina na muujiza utatendeka, sala haipaswi kuwafanya wawe wazubavu, haipaswi kuwafanya kushindwa kuwa na ndoto au malengo, sala haiwafanyi waamini wasiwe na upendo. Badala yake sala inawafanya waamini kuwa na tamaa ya kuwa na maisha, kuwa na siku nzuri, kuwa tayari kukabiliana na changamoto na kuwa na ujasiri wa kuendeleza ndoto zao na kuwashirikisha wengine upendo wa Mungu. Mungu hatuambii tusali kusudi tumlaumu pale tunaposhindwa katika maisha, bali tumtukuze na tumsifu pale maisha yanapofunguka na tunaposhinda. SALA: Mungu Mwenyezi utujalie tudumu katika sala na kutimiza wajibu wetu katika kazi kusudi neema zako zifuatane nasi katika kila tutendalo. |