Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 05/10/2024
2024 OKTOBA 5: JUMAMOSI-JUMA LA 26 LA MWAKA
Mt. Faustina Kowalska, Bikira
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma II
SOMO 1. Ayu 42: 1-3, 5-6, 12-17
Ayubu alimjibu Bwana na kusema, najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika. Ni nani huyu afichaye mashauri bila maarifa? Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua. Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; bali sasa jicho langu linakuona. Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu katika mavumbi na majivu. “Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng’ombe elfu, na punda wake elfu. Tena alikuwa na wana waume saba, na binti watatu. Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na wa pili akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu. Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wana waume. Kisha baada ya mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia na arobaini, naye akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hata vizazi vinne. Basi Ayubu akafa, mzee sana mwenye kujawa na siku. |
WIMBO WA KATIKATI. Zab 119: 66, 71, 75, 91, 125, 130
1. Unifundishe akili na maarifa, (K) “Umwangazie mtumishi wako uso wako, 2. Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki, 3. Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe, |
INJILI. Lk 10:17-24
Wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, “Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako.” Akawaambia, “Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.” Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza.” Akasema, “Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.” Akawageukia wanafunzi wake, akasema nao kwa faragha, “Heri macho yaonayo mnayoyaona ninyi. Kwa kuwa nawaambia ya kwamba manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi wasiyasikie.” |
TAFAKARI
ETI KWA SABABU: Katika yote tunayotenda na tuliyotenda, cha muhimu ni kwamba tumefanya kwa sababu imetupasa kufanya, hatuhitaji zawadi. Wanafunzi wanasoma kwa bidii kusudi wapate matokeo mazuri. Wafanyakazi wanafanya kazi hadi muda wa ziada kusudi wapate mshahara zaidi. Wafuasi wanamtumikia Mungu kusudi wapate kitu gani? Biblia inatuambia kwamba wafuasi wanapaswa kupiga hatua mbele zaidi kwa sababu wanampenda Mungu, na wanadamu, wanatimiza ahadi, wanamwabudu Mungu na kuwahubiria wengine kuhusu Yesu. Katika jitihada zako kwa ajili ya Kristo, mshukuru Mungu kwa sababu unayo ahadi ya maisha ya umilele. Sababu ya msingi iliyopelekea kumjua Mungu ni kwa sababu Mungu amekuchagu upate kumjua. Na kwa nini Mungu amefanya hivyo? Ni kwa sababu ya neema, zawadi ambayo tunaipata bure kwa upendo wake. Unapaswa kufanya nini basi? Mshukuru Mungu katika sala, ishi kwa ajili ya Mungu, zungumza mambo yamuhusuyo Mungu, na waoneshe wengine upendo wa Mungu. Zawadi kubwa anayopokea mtu huendana na kutoa shukrani kubwa. SALA: Ee Mungu tunakushukuru kwa kutuchagua; utujalie furaha ya kweli. |