
Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 20/03/2024
2024 MACHI 21 ALHAMISI: JUMA LA 5 LA KWARESIMA
Mt. Serapion
Urujuani
Zaburi: Juma 1
Somo 1. Mwa 17:3-9
Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako, nami nitakupa wewe na uzao baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao. Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako.
Wimbo wa Katikati. Zab 150:4-9
1. Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake siku zote.
Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya,
Miujiza yake na hukumu za kinywa chake. (K)
(K) Analikumbuka agano lake milele.
2. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake;
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
Duniani mwote mna hukumu zake. (K)
3. Analikumbuka agano lake milele;
Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.
Agano alilofanya na Ibrahimu,
Na uapo wake kwa Isaka. (K)
Injili. Yn 8:51-59
Yesu aliwaambia Wayahudi: Amin, amin, nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele. Basi Wayahudi wakamwambia, Sasa tumeng’amua ya kuwa una pepo. Ibrahimu amekufa, na manabii wamekufa; nawe wasema, Mtu akilishika neno langu, hataonja mauti milele. Wewe u mkuu kuliko baba yetu Ibrahimu, ambaye amekufa? Nao manabii wamekufa. Wajifanya u nani? Yesu akajibu, nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu; anitukuzaye ni Baba yangu, ambaye ninyi mwanena kuwa ni Mungu wenu. Wala ninyi hamkumjua; lakini mimi namjua. Nikisema ya kwamba simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi; lakini namjua, na neno lake nalishika. Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi. Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu? Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko. Basi wakaokota mawe ili wamtupie; lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni.
TAFAKARI
MUNGU YU TAYARI KUJIFUNUA KWETU: Kuna usemi usemao “Jambo usilolijua ni kama usiku wa kiza.” Katika Injili tumeona mabishano kati ya Yesu na Wayahudi juu ya kifo. Wayahudi kwa uelewa wao waliishia kwa kifo cha maisha ya dunia hii, Yesu alienda zaidi kumaanisha maisha ya umilele baada ya haya ya dunia hii na alionesha wazi kuwa maisha haya yanaashiria maisha yajayo na ni msingi kwa maisha ya umilele. Kuna watu katika jamii yetu ambao ni hodari kwa ubishi, unakuta mtu licha ya kwamba hana uhakika na jambo husika. Yesu alikuwa na uhakika na kile alichokuwa anafundisha. Kanisa sehemu nyingine limekwama kutokana na wachache kuwa wabishi bila sababu za msingi. Usishangae kusikia waamini wengine wanasema, ‘michango huku Kanisani imezidi,’ lakini watu hawa hawa wakihamia kwingineko wanakuwa watoaji wazuri tu. Hawa hawana tofauti na hawa Wayahudi wanaopingana na Yesu bila sababu za msingi.
SALA: Ee Mungu utuondolee roho wa ubishi maishani mwetu.