Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Juni 24

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 24/06/2024

2024 JUNI 24 : JUMATATU; JUMA  12 LA MWAKA

KUZALIWA MT. YOHANE MBATIZAJI
Rangi: 
Zaburi: Tazama Sala ya Siku

Somo 1. Isa 49:1-6

Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana ameniita tangu tumboni, toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali, katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha. Akaniambia, “Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa.” Lakini nikasema, “Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina Bwana, na thawabu yangu ina Mungu wangu.” Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya Bwana, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu; naam, asema hivi, “Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.”

Wimbo wa Katikati. Zab 139:1-3, 13-15

1. Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali,
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.

(K) Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa.

2. Maana wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.
Matendo yako ni ya ajabu. (K)

3. Na nafsi yangu yajua sana,
Mifupa yangu hakusitirika kwako,
Nilipoumbwa kwa siri,
Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi. (K)

Somo 2. Mdo 13: 22-26

Paulo alisema, Mungu alimwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, ‘nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote.’ Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi; Yohane alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake. Naye Yohane alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, ‘Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake.’ Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa.

Injili. Lk 1:57-66, 80

Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria.  Mamaye akajibu akasema, “La, sivyo; bali, ataitwa Yohane.” Wakamwambia, “Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo. Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. Akataka kibao, akaandika ya kwamba, ‘Jina lake ni Yohane’. Wakastaajabu wote. Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu. Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi. Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, “Mtoto huyu atakuwa wa namna gani?” Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli.

TAFAKARI

MAISHA MAADILIFU NI KIOO KWA JAMII: Mama Kanisa leo anaadhimisha tukio la kuzaliwa kwa mmoja wa manabii mashuhuri anayefunga Agano la Kale na kufungua Agano Jipya. Ni Yohane Mbatizaji, mwana wa Kuhani Zakaria na mkewe Elizabeti. Huyu ndiye mtangulizi wa Mwokozi Yesu Kristo. Kwa njia ya mahubiri yake na ubatizo wa toba, aliwatayarisha watu kumpokea Kristo. Huyu ndiye Yohane ambaye alimtambulisha Yesu kwa ulimwengu kama “Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu”(Yn 1:29). Alitoa maisha yake kwa kusema ukweli na kutetea maisha adilifu (rej. Mt 14:1-12). Tunaposherehekea sikukuu hii tunakumbushwa wajibu wetu wa kuwa sauti ya Kristo kwa kukemea maovu yanayotuzunguka na kutetea haki na kusema ukweli. Sisi sote tunaalikwa kuishi maisha maadilifu. Tumwombe Mt. Yohane Mbatizaji atuombee neema ya ujasiri ili nasi tuzaliwe upya kiroho. 

SALA: Ee Mungu utujalie fadhila ya uadilifu kama alivyokuwa Mt. Yohane Mbatizaji.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2023, 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you