Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 16/06/2024
2024 JUNI 16 : DOMINIKA YA 11 LA MWAKA
DOMINIKA YA 11 LA MWAKA
Rangi: Kiani
Zaburi: Tazama Sala ya Siku
Somo 1. Eze 17:22-24
Bwana Mungu asema hivi; mimi nami nitakitwaa kilele kirefu cha mwerezi, na kukipandikiza mahali; na katika vitawi vyake vilivyo juu nitatwaa kitawi kimoja kilicho chororo, nami nitakipanda juu ya mlima mrefu ulioinuka sana; juu ya mlima wa mahali palipoinuka pa Israeli nitakipanda; nacho kitatoa matawi, na kuzaa matunda, nao utakuwa mwerezi mzuri; na chini yake watakaa ndege wa kila namna ya mbawa; katika uvuli wa matawi yake watakaa. Na miti yote ya mashamba itajua ya kuwa mimi, Bwana, nimeushusha chini mti mrefu, na kuuinua mti mfupi, na kuukausha mti mbichi, na kuustawisha mti mkavu; mimi, Bwana, nimenena, nami nimelitenda jambo hili. |
Wimbo wa Katikati. Zab 92: 2-3, 13-16
1. Ni neno jema kumshukuru Bwana, (K) Ni neno jema kumshukuru Bwana. 2. Mwenye haki atasitawi kama mtende, 3. Watazaa matunda hadi wakati wa uzee, |
Somo 2. 2Kor 5:6-10
Siku zote tuna moyo mkuu; tena twajua ya kuwa, wakati tuwapo hapa katika mwili, tunakaa mbali na Bwana (maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona.) Lakini tuna moyo mkuu; nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana. Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye. Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya. |
Injili. Mk 4:26-34
Yesu alisema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara aupeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? au tuutie katika mfano gani? ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake. kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha. |
TAFAKARI
SISI NI WASIA MBEGU NA MUNGU NDIYE MKUZAJI WA MBEGU SALA: Ee Mungu utujalie neema ya kustawisha mbegu ya Ufalme wako ndani yetu. |