Jumamosi: Juma la I la Majilio
Kumbukumbu
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma I
Mt. Ambrosi Wa Milano, Askofu Na Mwalimu Wa Kanisa (340-397)
Utume: Ambrosi alizaliwa Ufaransa. Alipomaliza masomo yake ya sheria huko, aliwekwa kuwa Gavana wa Italia. Baada ya askofu wa Milano kufa, Ambrosi alipewa nafasi ya uaskofu wa jimbo hilo. Aliwagawia maskini mali zake na alianza kusoma Maandiko Matakatifu. Aidha aliwarudisha wafitini wengi wa dini katika imani katoliki.
SOMO 1. Isa 30:19-21, 23-26
Bwana Mungu Mtakatifu wa Israeli asema: watu watakaa katika Sayuni huko Yerusalemu; wewe hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu. Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako; na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto. Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng’ome zako watakula katika malisho mapana. Ng’ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo. Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara. Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile Bwana atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao.
SOMO 1. Zab 147:1-6
“1. Msifuni Bwana, maana ni vema kumwimbia Mungu wetu
Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri.
Bwana ndiye aijengaye Yerusalemu,
Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli.
(K) Heri wote wamngojao Bwana.
- Huwaponya waliopondeka moyo,
Na kuziganga jeraha zao.
Huihesabu idadi ya nyota,
Huzipa zote majina. (K) - Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu.
Akili zake hazina mpaka,
Bwana huwategemeza wenye upole,
Huwaangusha chini wenye jeuri. (K) “
INJILI. Mt 9:35 – 10:1, 5-8
Siku ile: Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Akawaambia, afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.
TAFAKARI
UTUME NA UMISIONARI: Utume unapata nguvu zake katika Yesu Kristo mwenyewe (alisukumwa na huruma) na katika sala ya wanakanisa. Makanisa ambayo yanategemea zaidi miradi ya maendeleo kuliko sala yanakosa nguvu katika utume na mwishoni kushindwa. Makanisa ambayo tamaa yao kubwa ni kuwasaidia waliopotea, au kuwaokoa wanaoangamia, wakiharakisha kufanya hivyo kwa sababu muda ni mchache, wanakuwa wamesahau kiini cha utume wa Yesu. Kiini cha mafanikio katika utume ni kuwa karibu zaidi na Yesu na kusali. Chiochote kanisa linachokifanya, lijifunze kupenda na kusali. Yesu aliwaita wafuasi wake, hakuwalazimisha, au kuwaomba wajitolee aliwachagua wamtumikie katika namna ya pekee. Yesu hakuwachagua hawa kumi na wawili kwa sababu ya imani yao, hakuwachagua kwa sababu ya vipaji vyao. Wafuasi walitoka katika mazingira mbali mbali na hawakuwa na taaluma yoyote ya uongozi. Sifa moja waliyokuwa nayo ni utayari wa kumtii Yesu. Yesu anatuita sisi leo. Tunapaswa kuamua sasa kumfuata au kubaki nyuma.
SALA: Bwana utusaidie kuisikia sauti yako na kukufuata kwa moyo wote.