Alhamisi: Juma la I la Majilio
Kumbukumbu ya Hiyari
Rangi: Urujuani
Zaburi: Juma I
SOMO 1. Isa 26:1-6
Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda; Sisi tunao mji ulio na nguvu; ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma. Wekeni wazi malango yake, taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie. Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini Bwana siku zote, maana Bwana Yehova ni mwamba wa milele. Kwa kuwa amewashusha wakaao juu, mji ule ulioinuka, aushusha, aushusha hata nchi, auleta hata mavumbini. Mguu utaukanyaga chini, naam, miguu yao walio maskini, na hatua zao walio wahitaji.
WIMBO WA KATIKATI. Zab 118:1, 8-9, 19-21, 25-27a
1. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema
Kwa maana fadhili zake ni za milele
Ni heri kumkimbilia Bwana
Kuliko kuwatumainia wanadamu
Ni heri kumkimbilia Bwana
Kuliko kuwatumainia watu.
(K) Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana.
2. Nifungulieni malango ya haki
Nitaingia na kumshukuru Mungu Bwana.
Lango hili ni la Bwana,
Wenye haki ndio watakaoliingia.
Nitakushukuru kwa maana umenijibu,
Nawe umekuwa wokovu wangu. (K)
3. Ee Bwana, utuokoe, twakusihi,
Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi,
Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana
Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana.
Bwana ndiye aliye Mungu
Naye ndiye aliyetupa nuru. (K)
INJILI. Mt 7:21, 24-27
Siku ile, Yesu akawaambia wafuasi wake: Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba, mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.
TAFAKARI.
MANENO MATUPU: Yesu hafurahishwi na wema au ukarimu usiotoka moyoni. Dini ambayo haina mizizi inakuwa inajishughulisha na mambo yanayoonekana ya kimwili. Lakini Yesu anataka utii unaoanzia ndani. Kusema “Bwana Bwana” pasipo kumtii Yesu ni kuvunja amri ya tatu: “Usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako.” Wako wengi wanaoshawishika kutokuwa waaminifu, na kufanya maigizo. Gamba la mambo ya kiroho yanaweza yakatulindia heshima yetu kwa watu lakini halitusaidii katika kukua kiroho. Tutakuwa tunajidanganya tukifikiri kwamba Mungu anaweza kudanganyika kwa utakatifu wa uongo. Mungu ni kweli na anapenda ukweli. Mungu anaona nini ndani ya maisha yako? Je, matendo yako yanaendana na maneno yako? Wanamichezo wengi wanaweza kuzungumzia mashindano makubwa waliyowahi ushindana lakini kamwe hawazungumzii ukweli wa kile kinachofanya washinde. Na sio wote wanaozungumzia ufalme wa Mungu ni wa ufalme wa Mungu. Yesu anazungumzia zaidi matendo yetu na sio maneno. Anataka tufanye yaliyo sahihi sio kuzungumzia yaliyo sahihi.
SALA: Bwana utusaidie maneno yetu yaendane na matendo yetu.