Jumatatu: Juma la 33
Kumbukumbu ya Hiyari
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma I
Mt. Hilda Wa Witbi, Mtawa (680)
Mtakatifu huyo, Mwingereza alibatizwa alipokuwa na umri wa miaka kumi na mitatu. Alipokuwa na miaka thelathini na mitatu, aliamua kumtumikia Mungu utawani. Aliwekwa kuwa mama abati wa monasteri kubwa. Mwaka 657 alianzisha upya monasteri kule Witbi (Uingereza).
SOMO 1. Ufu 3:1-6, 14-22
Mimi Yohane, nilisikia Bwana anayeniambia: kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa. Uwe mwenye kukesha, ukayaimarishe mambo yaaliyosalia, yanayotaka kufa. Maana sikuona matendo yako kuwa yametimilika mbele za Mungu wangu. Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako. Lakini unayo majina machache katika Sardi, watu wasioyatia mavazi yao uchafu. Nao watakwenda pamoja nami hali wamevaa mavazi meupe, kwa kuwa wamestahili. Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri; na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane; na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu. Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.
WIMBO WA KATIKATI. Zab 15:1-4, 5
“1. Bwana, ni nani atakayekaa
Katika hema yako?
Ni mtu aendaye kwa ukamilifu,
Na kutenda haki.
(K) Yeye ashindaye, nitamketisha pamoja nami.
- Asemaye kweli kwa moyo wake,
Asiyesingizia kwa ulimi wake.
Wala hakumtenda mwenzie mabaya.
Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
Bali huwaheshimu wamchao Bwana. (K) - Hakutoa fedha yake apate kula riba,
Hakutwa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo hataondoshwa milele. (K)
“
INJILI. Lk 19: 1-10
Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake. Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kupitia njia ile. Naye Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu walipoona, walinung’unika wote, wakisema, ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimemnyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.
TAFAKARI
UPENDO KWA WOTE: Watozaushuru walikuwa ni watu wasiopendwa katika Israeli. Walikuwa ni Wayahudi kwa asili lakini walichagua kufanya kazi kwa ajili ya Warumi, na kwa sababu hiyo walikuwa wakionekana kuwa ni wasaliti wa taifa lao. Lakini pia ilikuwa inajulikana wazi kwamba watoza ushuru walikuwa wakijikusanyia mali kwa kuwatoza zaidi Wayahudi wenzao. Hii ndiyo sababu watu walishangaa Yesu alipokwenda katika nyumba ya mkuu wa watoza ushuru Zakayo. Pamoja na ukweli huu kwamba Zakayo alikuwa akidanganya watu, Yesu alimpenda na kwa matokeo yake Zakayo aliongoka. Katika jamii yoyote kuna makundi ya watu yaliyokuwa yakitengwa pengine kutokana na msimamo wao katika siasa, tabia mbaya, au mtindo wa maisha. Tusifuate mkumbo wa jamii na kuwakwepa watu kama hao. Yesu aliwapenda na wanahitaji kusikia Habari hii njema. Ni Yesu aliyepiga hatua ya kwanza kumwendea Zakayo. Alipita katikati ya tabia ya kuwabagua watu waliyonayo wayahudi. Tukwepe kuwahukumu watu kulingana na jamii inavyosema.
SALA: Ee Mungu utujalie moyo wa kuwapenda na kuwaona watu wote kama wana wako.