Masomo ya misa

Msomo ya Misa: Novemba 20

By

on

Jumatatu: Juma la 33
Kumbukumbu ya Hiyari
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma I

Mt. Andrea Avelino, Mtawa (1521-1608)

Utume:  Alipopewa Upadre kwanza alisomea sheria, kisha akawa wakili katika baraza la Kanisa. Neema ya Mungu ilimsaidia kuongoza roho za watu, hasa wakati wa kuungamisha, Mungu alimfumbulia siri zao. Mahubiri yake katika makanisa yaliwaongoa wengi.

SOMO 1. Ufu 4:1-11

Mimi, Yohane, niliona mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo. Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti; na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi. Na viti ishirini na vinne, vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu. Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zilikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu.  Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma. Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa Mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye.  Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema: Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja. Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele, ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao umsujudia yeye alie hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi, wakisema, Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 150: 1-6

“1. Aleluya.
Msifuni Mungu katika patakatifu pake,
Msifuni katika anga la uweza wake.
Msifuni kwa matendo yake makuu;
Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.

(K) Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi.

  1. Msifuni kwa mvumo wa baragumu;
    Msifuni kwa kinanda na kinubi;
    Msifuni kwa matari na kucheza;
    Msifuni kwa zeze na filimbi. (K)
  2. Msifuni kwa matoazi yaliayo;
    Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.
    Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana.
    Aleluya. (K)”

INJILI. Lk 19:11-28

Makutano waliposikia, Yesu aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara. Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi. Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja. Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale. Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake. Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi. Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi. Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida. Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano. Akaja mwingine akasema, Bwana hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso, Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda. Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda; basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake? Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang’anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi. Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi, Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho. Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu. Na alipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu.

TAFAKARI

ANGALIZO, SIKILIZENI: Watu walifanya vyema kumsikiliza Yesu, lakini walichokuwa wakisikia sio ujumbe wake, bali kile walichokuwa wakitarajia ni kile walichokuwa wakitaka wao, yaani kiongozi atakayewaondoa Warumi. Ni rahisi sana kuyaamishia mahitaji na matakwa yetu kwa Yesu. Je, unaposikia Neno la Mungu likifundishwa au kuhubiriwa, mara moja unalitafakari kulingana na mambo yako? Chuja mambo yasiyoendana na matamanio yako. Mungu analeta changamoto katika maisha yetu lakini kwanza tunapaswa kusikiliza na kujifunza. Usiyaweke maneno ya Mungu katika kabati la maisha yako, litumie neno hilo. Angalizo la kusikiliza maana yake tumsikilize Mungu hata kama tumeziba masikio yetu kwa ubinafsi, ubaguzi, na kuwadhani wengine vibaya. Inahitaji utayari katika kutenda. Tatizo la yule aliyepokea talanta moja ni kumpa ahadi ya maneno bwana wake (yaani alikubali kufanya kazi ile), lakini hakufanya jitihada zozote. Yesu hatawakemea wafuasi wake kwa kujaribu kutumia kile walichopewa hatakama kinaweza kuwatia hasara au kushindwa bali kwa kukosa uaminifu.

SALA: Bwana utujalie tuwe na uthubutu wa kuvitumia vipaji ulivyotujalia.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2025 2024 2023 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you