Ijumaa: Juma la 33
Kumbukumbu
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Juma I
Mt. Sesilia, Mfiadini (karne Ya Tatu)
Utume: MT.Sesilia alikuwa mfiadini, aliyeuawa kwa sababu ya Upendo wake kwa Kristu. Aliingia Ukristu na kuweka nadhiri ya Ubikira. Mt.Sesilia alifunga na kusali kupata msaada wa Mungu katika Masumbuko yake.
SOMO 1. Ufu 10:8-11
Mimi, Yohane, nilisikia sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi. Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali. Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu. Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi.
WIMBO WA KATIKATI. Zab 119:14, 24, 72, 103, 111, 131
“1. Nimeifurahia njia ya shuhuda zako,
kana kwamba ni mali mengi.
Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu,
na washauri wangu.
(K) Mausia yako ni matamu sana kwangu.
- Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
Mausia yako ni matamu sana kwangu,
kupita asali kinywani mwangu. (K) - Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele,
maana ndizo changamko la moyo wangu.
Nalifunua kinywa changu nikatweta,
maana naliyatamani maagizo yako. (K)
“
INJILI. Lk 19:45-48
Yesu aliingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi. Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza; wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye, wakimsikiliza.
TAFAKARI.
NYUMBA YA SALA: Yesu alisema kwamba hekalu linapaswa kuwa nyumba ya sala. “Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.” Watu wanaelezaje kanisa lako au kanisa lenu? Je, ni sehemu ya kukutanika vikundi vya vijana, ambapo wanapata fedha fulani kwa ajili ya kujikimu? Je, ni sehemu ambapo watu wanapatiwa ushauri mzuri kuhusu maisha familia, hasa ndoa na malezi au sehemu ya kutolea semina na warsha mbali mbali? Ni sehemu ambapo kuna kwaya nzuri sana yenye nyimbo za kisasa zinazochangamsha waamini na vifaa vizuri vya muziki? Na vipi je, kuhusu nyumba ya sala? Je, kanisa limekuwa sehemu ya minada zaidi? Je, wafanya biashara wamegeuza kanisa lenu kutoka katika lengo lake yaani nyumba ya sala? Utafanya nini kusudi uweze kuelewa vyema kuhusu sala? Je unafanya mazoezi ya sala na kusali mara kwa mara? Unawaongoza watu wengine kanisani na kuipatia sala kipaumbele au nafasi ya kwanza.
SALA: Ee Bwana utujalie kuheshimu nyumba yako na kamwe tusisahau kwamba ni mahali pa sala.