Jumatatu: Juma la 33
Kumbukumbu
Rangi: White
Zaburi: Juma 4
Kutabarukiwa Mabasilika ya Wat. Petro na Paulo, Mitume
Zamani sana, kanisa lilijengwa juu ya kaburi la Mt. Petro, Mtume. Vile vile juu ya kaburi la Mt. Paulo, Mtume huko Roma. Liturjia inaadhimisha kutabarukiwa kwa mabasilika haya mawili. Kama vile adhimisho la kutabarukiwa kanisa kuu la Mama Maria. Imani waliyoitangaza mitume hao, ndiyo imani yetu pia.
SOMO 1. SOMO I: Mdo 28: 11-16, 30 au (Ufu. 4:1-11)
Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Iskanderia iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha. Tukafika Sirakusa, tukakaa siku tatu. Kutoka huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na siku ya pili tukawasili Puteoli. Huko tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi tukafika Rumi. Na kutoka huko ndugu, waliposikia habari zetu, wakaja kutulaki mpaka Soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akachangamka. Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda. Akakaa muda wa miaka miwili mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 98: 1-6 au (Zab. 150)
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Bwana ameidhihirisha haki yake Machoni pa mataifa.
Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu.
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana. (K)
SHANGILIO Mt. 4: 19
Aleluya, aleluya,
Ee Mungu, tunakusifu, tunakukiri,
kuwa Bwana, jamii tukufu ya mitume inakusifu.
Aleluya.
INJILI: Mt. 22-33 au (Lk. 19:11-28)
Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.
VIPAJI VYETU VITUMIKE VYEMA: Mungu alipotuumba wanadamu, kila mmoja alipewa uwezo na zawadi ya kuwa wa muhimu kadiri ya uwezo na nafasi yake katika jamii. Hivyo kila mmoja anacho kipaji na ujuzi aliozawadiwa, na katika hivyo tutapaswa kutolea hesabu ya utendaji kazi wetu. Uwezo na vipaji vyetu sio vyakufungiwa au kuchimbiwa chini bali ni vyakutumiwa ili kuweza kuzalisha zaidi na zaidi. Kufukia chini vipaji vyetu ni sawa na kumkosoa Mungu na kumuonesha kwamba alikosea kutujalia hivyo vipaji. Woga siku zote umekuwa ni mwiba unao kwamisha maendeleo katika maisha yetu. Woga unatoka kwa mwovu shetani na ujasiri hutoka kwa Mungu aliyetujalia uwezo wa kufanya yaliyo mema. Tuukumbatie ujasiri na kutupilia mbali woga. Tukivitumia vyema vipaji vyetu kwaajili yetu na ya wenzetu, na tukimtanguliza na kumuishi Kristo, basi tumalizapo safari yetu hapa duniani tutaungana na wale wenye uhai wanne tukisema “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi”.
SALA: Ee Mungu mpaji wa vipaji vyote, tujalie moyo wa ujasiri kuweza kutumia vyema vipaji vyetu, amina.