Kumbukumbu
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: 2 Yoh 1: 4-9
Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba. Na sasa, mama, nakuomba, si kwamba nakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo, kwamba tupendane. Na huu ndio upendo; tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo. Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo. Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu. Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia.
WIMBO WA KATIKATI: Zab 119:1-2, 10-11, 17-18
“1. Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote.
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.
- Kwa moyo wangu wote nimekutafuta
Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.
Moyoni mwangu nimeliweka neno lako,
Nisije nikakutenda dhambi. (K) - Umtendee mtumishi wako ukarimu,
Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.
Unifumbue macho yangu niyatazame
Maaajabu yatokayo katika sheria yako. (K)”
INJILI: Lk 17:26-37
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulikunya moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu. Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya. Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai.
TAFAKARI
JIWEKENI TAYARI: Kristo atakuja ghafla bila taarifa. Baadhi ya watu watakuwa wakiendelea na shughuli zao za kila siku na kupuuzia habari za Mungu. Watapigwa na mshangao kwa ujio wake kama ilivyokuwa kwa watu wa kipindi cha Nuhu, au kama kwa watu wa siku za Lutu walivyoshangazwa pale Sodoma ilipoharibiwa. Hakuna ajuaye Kristo atakuja lini, lakini ujio wake ni wa hakika. Anaweza akaja leo au kesho au karne zijazo. Yesu atakapokuja waamini wanapaswa kuwa wamejiweka tayari kiroho na kimaadili. Tuishi kana kwamba Yesu anakuja leo. Tuyapoteze maisha kusudi tuyaokoe. Wale wanaoyang’ang’ania maisha haya ni wale ambao wanayakimbia madhulumu. Wale wanaoishi kwa ajili yao wenyewe ndio hao wanaoonesha tabia au maelekeo haya: Kupenda mali: Nakitaka hiki na nitafanya juu chini nikipate. Ubinafsi: Ninafanya kazi kwa bidii kwa ajili yangu mwenyewe. Ninaweza kufanikiwa. Huwezi kufanikiwa. Hilo ni shauri lako. Watu wenye tabia hizi wanajilinda wao wenyewe na kupoteza mambo ya kiroho katika maisha yao.
SALA: Bwana tunaomba utujalie kujiweka mikononi mwako kusudi tuwe tayari utakaporudi tena.