Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Juni 27

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 27/06/2024

2024 JUNI 27: ALHISI; JUMA  12 LA MWAKA

Sirili wa Alexandria, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Rangi: 
Zaburi:

Somo 1. 2 Fal 24:8-17

Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, mfano wa yote aliyoyafanya baba yake. Wakati ule watumishi wa Nebukadreza mfalme wa Babeli wakakwea kwenda Yerusalemu, na mji ukahusuriwa. Na Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akaufikilia huo mji, hapo watumishi wake walipokuwa wakiuhusuru. Na Yekonia, mfalme wa Yuda, akatoka, akamwendea mfalme wa Babeli, yeye na mama yake, na watumishi wake, na wakuu wa watu wake, na maakida wake; mfalme wa Babeli akamchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake. Akatoa huko hazina zote za nyumba ya Bwana, na hazina za nyumba ya mfalme, akavikata-kata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani, mfalme wa Israeli, alivifanya katika hekalu la Bwana, kama Bwana alivyosema. Akawachukua mateka watu wa Yerusalemu wote pia, na wakuu wote, na mashujaa wote, watu elfu kumi; na mafundi wote, na wafua chuma wote; hapana mtu aliyebaki, ila waliokuwa wanyonge, na watu wa nchi. Akamchukua Yekonia mpaka Babeli; na mama yake mfalme, na wake zake mfalme, na maakida wake, na wakuu wa nchi, aliwachukua mateka toka Yerusalemu mpaka Babeli. Na mashujaa wote, watu elfu saba, na mafundi, na wafua chuma elfu moja, na wote pia wenye nguvu, tayari kwa vita, hao wote mfalme wa Babeli aliwachukua mateka mpaka Babeli.  Mfalme wa Babeli akamtawaza Matania, ndugu ya baba yake, awe mfalme badala yake, akalibadili jina lake, akamwita Sedekia.

Wimbo wa Katikati. Zab 79: 1-5, 8-9

1.  Ee   Mungu, Mataifa wameingia katika urithi wako,
    Wamelinajisi hekalu lako takatifu.
    Wamefanya Yerusalemu chungu chungu,
    Wameziacha maiti za watumishi wako
    Ziwe chakula cha ndege wa angani.
   Na miili ya watauwa wako
    Iwe chakula cha Wanyama nchi.

(K) Utuokoe Ee Bwana, kwa ajili ya jina lako.

2. Wamemwaga damu yao kama maji
    Pande zote za Yerusalemu,
    Wala hapakuwa na mzishi.
   Tumekuwa lawama kwa jirani zetu,
   Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.
   Ee Bwana, hata lini? Utaona hasira ya milele?
   Wivu wako utawaka kama moto? (K)

3.  Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
     Rehema zako zije kutulaki hima.
      Kwa maana tumeridhika sana. (K)

4.  Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie,
     Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
    Utuokoe, utughofiri dhambi zetu,
    Kwa ajili ya jina lako. (K)

Injili. Mt 7:21-29

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa. Ikawa, Yesu alipoyamaliza maneno hayo, makutano walishangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi wao.

TAFAKARI

MATENDO HUKIDHI HAJA MARIDHAWA KULIKO MANENO: Injili ya leo ni mwendelezo wa Injili ya jana. Tunafundishwa kuwa haitoshi tu kusema na kuimba matakatifu bali ni muhimu zaidi kuishi na kuweka katika matendo yale tunayosema na kuimba kumhusu Mungu. Tunafundishwa pia kuwa jumuiya iliyojengwa vizuri juu ya imani itasimama imara hata katika nyakati ngumu za mateso. Mfano mzuri watakatifu mashahidi ambao kutokana na imani yao kwa Mungu waliweza kusimama imara katika imani yao, hata wakati wa madhulumu hawakutikisika. Tunakumbushwa pia kuwa haitoshi kuongea vizuri tu kuhusu Mungu, kuchambua vizuri Neno la Mungu, kuhubiri vizuri bali kutimiza mapenzi ya Mungu. Tusiwe watu wa kuongea mambo yamhusuyo Mungu na kutenda kinyume chake. Katika Injili ya Mtakatifu Luka tunasoma “Lakini heri zaidi wale wanaolikisikia neno la Mungu na kulishika” (Lk. 11:28). Hili ni jibu la Yesu kwa mama aliyesifia utendaji wa Yesu. Kwa jibu hili la Yesu ni wazi kuwa tunapewa mwaliko wa kutenda zaidi kuliko kuongea. 

SALA: Ee Yesu unijalie kutenda kwa kadiri ya mapenzi yako.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2023, 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you