Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Juni 11

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 11/06/2024

2024 JUNI 11 : JUMANNE-JUMA LA 10 LA MWAKA

Mt. Barnaba, Mtume
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku

Somo 1. Mdo 11:21-26, 13:1-3

Watu wengi waliamini, wakamwelekea Bwana. Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia. Naye alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana. Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.  Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na walimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Maneani aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.

Wimbo wa Katikati. Zab 98:1-6

1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana amatenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umetenda wokovu.

(K) Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa.

2. Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)

3. Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)

4. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu.
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana. (K)

Injili. Mt.  10:7-13

Yesu aliwaambia mitume wake, katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.  Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo;  mmepata bure, toeni bure.  Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake. Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka.  Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni.  Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi.

TAFAKARI

SISI NI CHUMVI, SISI NI NURU: Chumvi ni kiungo kidogo katika chakula ila kina umuhimu mkubwa sana. Chumvi ikikosekana katika chakula, chakula kinakosa ladha. Chumvi haipo kwa ajili yake tu bali kwa ajili ya kukoleza chakula na kutunza vitu visiharibike. Kadhalika taa haipo kwa ajili yake yenyewe bali ipo kwa lengo la kuondoa giza na kuwaangazia watu. Maisha yetu sisi wabatizwa ni maisha yanayopaswa kuleta ladha na mwanga katika jamii tunamoishi. Elimu nzuri na ufunuo tuliojaliwa na Mungu kuhusu ufalme wa Mbinguni vinapaswa kuijenga jamii. Tusipofanya hivyo maovu yatatawala duniani. Maisha ya Mkristo yanapaswa kuwafanya watu wamwone Kristo, wamwonje na kumpenda. Mtakatifu Barnaba tunayeadhimisha sikukuu yake leo alikuwa chumvi na mwanga katika jamii. Maisha yake yaliwagusa wengi katika jamii wakapata wokovu. Tumwombe mtakatifu huyu atuombee nasi maisha yetu yaweze kuleta ladha na mwanga katika jamii.

SALA: Ee Yesu nijalie niweze kuleta ladha na mwanga katika jamii.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2023, 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you