Ijumaa: Juma la I la Majilio
Kumbukumbu ya Hiyari
Rangi: Urujuani
Zaburi: Juma I
Mt. Nikolao, Askofu
SOMO 1. Isa 29:17-24
Bwana Mungu asema: je! Si muda mdogo uliobaki, na Lebanoni itageuzwa kuwa shamba lizaalo sana, na lile shamba lizaalo sana litahesabiwa kuwa msitu? Na katika siku hiyo viziwi watasikia maneno ya hicho chuo, na macho ya vipofu yataona katika upofu na katika giza. Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika Bwana, na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli. Kwa maana mwenye kutisha ameangamizwa, naye mwenye dharau amekoma, nao wote watazamiao uovu wamekatiliwa mbali; hao wamfanyao mtu kuwa amekosa katika neno, na kumtegea mtego yeye aonyaye langoni, na kumgeuza mwenye haki kwa kitu kisichofaa. Basi, Bwana aliyemkomboa Ibrahimu asema hivi, katika habari za nyumba ya Yakobo; Yakobo hatatahayarika sasa, wala uso wake hautabadilika rangi yake. Bali atakapowaona watoto wake, walio kazi ya mikono yangu, katikati yake, wao watalitakasa jina langu; naam, watamtakasa Mtakatifu wa Yakobo, nao watamcha Mungu wa Israeli. Hao nao wakosao rohoni mwao watapata kufahamu, na hao wanung’unikao watalifunza elimu.
WIMBO WA KATIKATI. Zab 27:1, 4, 13-14
“1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K) Bwana ni nuru na wokovu wangu.
- Neno moja nimelitaka kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana
Siku zote za maisha yangu.
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake. (K) - Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K) “
INJILI. Mt 9:27-31
Siku ile: Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi. Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana. Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate. Macho yao yakafumbuka. Naye Yesu akawaagiza kwa nguvu, akisema, Angalieni hata mtu mmoja asijue. Lakini wakatoka, wakaeneza habari zake katika nchi ile yote.
TAFAKARI
NDIYO BWANA: Ni jambo rahisi kabisa lakini la kina. Vipofu wameonesha imani yao kwa maneno dhahiri kwa kusema, “Naama Bwana.” Tunaposema amina kila tunapofunga sala zetu, ni sawa sawa na kusema ndiyo Bwana. Amina sio hitimisho la sentensi. Ni kama kura ya kusadiki au kuwa na matumaini kwamba Yesu Bwana wetu anaweza kutenda. Tuifanye “amina” yetu iwe na nguvu. Ni kama kumfuata Yesu hadi nyumbani na kumwomba atusaidie. Msaada mara nyingi unatuonesha maana yake. Kila mara tunapomaliza sala zetu, tumalizie kwa kusema “Naam Bwana weweza.” Kuna wakati tunafikiri kwamba uongofu/kuokoka kunaondoa matatizo na changamoto zetu, kwa sababu wale waliookoka wanamtii Yesu na kuishi kadiri ya amri zake. Lakini hapa tunawaona vipofu wawili waliojaa imani wanaponywa, na mara moja wanaacha kutii agizo; “angalieni hata mtu mmoja asijue.” Kuna wakati tunaruhusu furaha yetu ituongoze badala ya kusikiliza maneno ya Yesu. Ama tunafikiri kwamba tunajua zaidi na kupuuzia maneno ya Yesu. Tuyachukulie maneno ya Yesu katika uzito wake na kuyaishi.
SALA: Bwana Yesu utufanye watiifu kwa neno lako na tukupatie wewe nafasi ya kwanza katika maisha yetu.