Masomo ya misa

Masomo ya Misa Disemba 3

By

on

Jumane: Juma la I la Majilio
Kumbukumbu
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma I

SOMO 1. Isa 11:1-10

Siku ile litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia. Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakula pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe. Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira. Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari. Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzika patakuwa na utukufu.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 72: 1-2, 7-8, 12-13,17

1. Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
Na mwana wa mfalme haki yako
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu.

(K) ” Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi
na wingi wa amani kwa milele. “

2. Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi
            Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
            Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
            Toka Mto hata miisho ya dunia. (K)

3. Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
            Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi
             Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
             Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)

4. Jina lake na lidumu milele,
            Pindi ling’aapo jua jina lake liwe na wazao;
            Mataifa yote na wajibariki katika yeye,
            Na kumwita heri. (K)

INJILI. Lk 10:21-24

Siku ile, Yesu alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza. Akasema, nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia. Akawageukia wanafunzi wake, akasema nao kwa faragha, Heri macho yaonayo mnayoyaona ninyi. Kwa kuwa nawaambia ya kwamba manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi wasiyasikie.

TAFAKARI

WEWE NI CHAGUO LA MUNGU: Umewezaje kumjua Mungu? Kwa mkristo wa kawaida kabisa anaweza kusema ni katika kusoma Biblia, au kuna mtu alinishuhudia. Lakini sababu msingi ni hii kwamba Mungu amekuchagua kusudi umjue. Kwa nini Mungu amefanya hivyo? Sio kwa sababu umekuwa mwema sana bali ni kwa sababu ya neema yake, ambayo ni zawadi ya upendo kwako. Unapaswa kufanya nini basi? Mshukuru Mungu kwa sala. Kila siku unayoishi, ishi kwa ajili ya Mungu. Zungumza kuhusu Mungu na uoneshe upendo wa Mungu kwa kuwa mkarimu kwa wengine. Wafuasi walipata fursa ya pekee kabisa. Wao walimwona Kristo kwa macho yao lakini wengo wao walimchukulia kawaida tu. Wakati mwingine hawakumsikiliza wala kumtii. Sisi waamini siku hizi pia tunayo fursa. Tumekuwa na uelewa mpana uliojengeka kwa miaka zaidi ya elfu mbili katika historia ya kanisa. Lakini hata hivyo wakristo tulio wengi tunachukulia hilo katika hali ya kawaida kabisa. Tukumbuke kwamba upendeleo unakuja na wajibu. Tunapaswa kuwa waangalifu  na kumfuata.

SALA: Bwana nakushukuru kwa sababu umenichagua na kuniweka katika Kanisa lako.

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2025 2024 2023 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you