Masomo ya misa

Masomo ya Misa: Novemba 25

By

on

Jumatatu: Juma la 34
Kumbukumbu ya Hiyari
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma II

SOMO 1. Ufu 14:1-5

Mimi, Yohane, niliona, na tazama, huyo Mwanakondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu mia na arobaini na nne elfu pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao. Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni, kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu. Na hiyo sauti niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi, wakivipiga vinubi vyao; na kuimba wimbo mpya mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele ya wale wenye uhai wanne, na wale wazee; wala hapana mtu aliyeweza kujifunza wimbo ule, ila wale mia na arobaini na nne elfu, walionunuliwa katika nchi. Hawa ndio wasiotiwa unajisi pamoja na wanawake, kwa maana ni bikira. Hawa ndio wamfuatao Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa mwana-kondoo. Na katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 24:1-6

“1. Nchi navyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.

(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.

  1. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
    Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
    Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
    Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili,
    Wala hakuapa kwa hila. (K)
  2. Atapokea baraka kwa Bwana,
    Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
    Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
    Wakutafutao uso wako, Ee Bwana wa Yakobo. (K)”

INJILI. Lk 21:1-4

Yesu aliinua macho yake akawaona matajiri wakitia sadaka zao katika sanduku la hazina. Akamwona mjane mmoja maskini akitia mle senti mbili. Akasema, Hakika nawaambieni, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote; maana, hao wote walitia sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo.

TAFAKARI

NI ZAIDI YA USHAWISHI: Mjane huyu alitoa chote alichonacho nayo ni riziki yake ya siku. Hii ni tofauti kabisa na watu wengine walivyofanya na pesa zao. Wale wanaofikiria kutoa asilimia fulani ya mapato yao na kuona wamefanikiwa sana, wanafanana na wale waliotoa mali zao. Yesu alisifu namna ile ya kutoa kwa kujisadaka na kwa ukarimu, iwe ni muda wao, pesa, na hata vipaji. Wewe unajisikiaje unapoona chombo cha sadaka kinakuja mbele yako au unapofika wakati wa kutoa sadaka au michangao mingine? Unajisikia unakwazika, unapiga miayo na moyo unaenda mbio? Mama mjane amekufundisha kutoa hata kidogo kwa ukarimu kwa ajili ya kueneza ufalme wa Mungu katika kanisa lako ukijua kwamba Mungu atafanya mambo makubwa kwa mchango wako mdogo. Huo ndio ujumbe anaotupatia Luka muinjili. Matoleo ya yule mjane yalizidi matoleo ya wale wote kwa sababu alitoa kwa ukarimu na kwa kujisadaka, wakati wengine walitoa kwa kujionesha tena kile kilichowazidia. Kwa kawaida Mungu anaheshimu kutoa kwa namna gani? Je, wewe unafanana na nani katika utoaji?

SALA: Ee Mungu utujalie ukarimu kwa mapaji yale uliyotujalia, tukijua kwamba yote tumeyapokea kutoka kwako. 

About mzigotv

Nyimbo Mpya 2025 2024 2023 2022 Download Audio, Video, Mp3, Mp3 African music, Tanzania Music, Naijamusic, naijavibe, Bekaboy, Djmwanga, Tanzania songs, Kenya songs, Uganda songs, Rwanda songs, Congo songs, Zanzibar, Singeli, Taarabu, Reggae, Amapiano, Nyimbo za dini, Gospel songs, Diamond platnumz, jux, Rayvanny, Harmonize, Nandy, Zuchu, Wasafi, Alikiba Teading songs, Top 100 songs youtube, Nigeria, Naija songs.

Recommended for you