Alhamisi: Juma la 33
Kumbukumbu
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma I
Kutolewa Bikira Maria Hekaluni
Ionekanavyo, msingi wa adhimisho la leo ni kwamba kanisa la Bikira Maria kule Yerusalemu, lilitabarukiwa mwaka 543. Maria akiwa angali mtoto alipelekwa hekaluni na wazazi wake, kufuatana na nadhiri yao ya kumtolea Mungu mtoto wao. Alipendelea sana kusali. Sikukuu hii yatusaidia kukumbuka kwamba tangu miaka yake ya kwanza, Maria alimwelekea Mungu.
SOMO 1. Ufu 5:1-10
Mimi, Yohane, niliona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba. Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, N’nani astahiliye kukifungua kitabu, na kuzivunja muhuri zake? Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba. Nikaona katikati ya kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote. Akaja, akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi. Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu. Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.
WIMBO WA KATIKATI. Zab 149:1-6, 9
“1. Aleluya.
Mwaimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
(K) Ulitufanya kuwa wafalme na makuhani.
- Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapambana wenye upole kwa wokovu. (K) - Watauwa na washangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mung una ziwe vinywani mwao,
Hiyo ndio heshima ya watauwa wake wote.
Aleluya. (K)”
INJILI. Lk 19:41-44
Yesu alipofika karibu ya Yerusalemu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe, katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.
TAFAKARI
SIKU NDIYO HII: Imani ya kikristo inaonekana kuwa ni mchakato mrefu sana, mchakato ambao unahitaji mambo mengi na unahitaji maisha ya mtu. Injili inatuonesha kwamba Neno la Mungu limehubiriwa kwa wenyeji wa Yerusalemu kwa karne nyingi lakini matunda yake sio ya kuridhisha kabisa, kiasi kwamba Yesu aliulilia mji wa Yerusalemu na watu wake kwa sababu walishindwa kuuona ukweli wa Mungu. Wale waliochelewa kujitoa kwa Kristo wanafanya makosa yale yale waliyofanya wenyeji wa Yerusalemu. Kumbe basi ni jukumu letu kuwatia moyo wengine wasiahirishe kumpokea Kristo kana kwamba Yesu anapewa nafasi ya pili katika maisha. Kitendo chao cha kumpokea kama mkombozi wao ni cha muhimu sana, na majitoleo yao kwa ufalme wa Mungu unahitajika. Watu wanahitaji sana amani hii ambayo Kristo anaitoa. Tunawajibu wa kuwashirikisha watu zawadi ya habari njema ya Mungu. Tuwashauri waipokee zawadi hiyo kabla fursa haijapita.
“SALA: Bwana tunaomba neema ya kuwashirikisha wengine ujumbe wako kusudi waweze kukupokea wewe kama Bwana na Mkombozi wao.”