Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 22/10/2024
2024 OKTOBA 22: JUMANNE: JUMA LA 29 LA MWAKA
Mt. Papa Yohane Paulo II / Maria Salome
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma I
SOMO 1. Efe 2:12-22
Msisahau kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio na maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani. Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndio sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani. Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba. Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu. Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja. Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho. |
WIMBO WA KATIKATI. Zab 85:9-14
1. Nisikie atakavyosema Bwana, (K) Bwana anawaambia watu wake amani. 2. Fadhili na kweli vimekutana, 3. Bwana atatoa kilicho chema, |
INJILI. Lk 12:35-38
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara. Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia. Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao. |
TAFAKARI
TUSUBIRI NA TUWE TAYARI: Kujiweka tayari kwa ujio wa Kristo ni kuishi katika ulimwengu huu na ulimwengu mwingine kwa wakati huo huo. Ulimwengu wa kwanza ni huu wa nyakati na mahali. Ni mahali ambapo watu wa Mungu wanasaidiana na kuutunza ulimwengu. Ulimwengu mwingine ni ule ambao ulifanywa upya kwa ujio wa Yesu Kristo ambao maandalizi yake yanajumuisha sala, kuabudu, na kusoma Maandiko Matakatifu. Tunawezaje kujiweka tayari kwa ujio wa Yesu Kristo? Wale wanaojiweka tayari wanakuwa wawazi, hawana woga bali wako tayari wakati wote kutoa ushuhuda wa matendo yao mema na matendo makuu ya Mungu. Hawana mashaka bali wakati wote wanamtumainia Mungu. Sio wavivu bali wachapakazi daima. Maisha yetu yafanane zaidi na Kristo kusudi atakapokuja tuweze kumpokea kwa furaha. “Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao.” SALA: Ee Bwana ujujalie siku zote tujiweke tayari kwa siku tutakayokutana nawe katika kifo. |